Feb 19, 2014

Rwanda yapongeza hukumu ya Rwabukombe huko Ujerumani

Onesphore Rwabukombe, mwenye suti ya kijivu akipigwa picha na wanahabari huko Frankfurt, Germany, 18 Jan 2011
Onesphore Rwabukombe, mwenye suti ya kijivu akipigwa picha na wanahabari huko Frankfurt, Germany, 18 Jan 2011

Mahakama moja ya Ujerumani imemhukumu meya wa zamani wa Rwanda, Onesphore Rwabukombe, kifungo cha miaka 14 gerezani kwa jukumu lake katika mauaji ya halaiki ya  mwaka 1994 ya Rwanda.
 

Mauaji ya halaiki Rwanda, 1994 Rwabukombe  mwenye umri wa miaka 56 alikutwa na hatia ya kuamuru mauwaji ya  mamia ya watu katika kanisa moja ambako watu  walikusanyika kupata hifadhi huko Kiziguro. Amekuwa akiishi kama mkimbizi wa kisiasa nchini Ujerumani tangu mwaka 2002.
Hii ni kesi ya kwanza kufanyika Ujerumani iliyohusisha mauaji ya halaiki nchini Rwanda. Kesi hiyo iliyodumu miaka mitatu huko Frankfurt ilisikiliza ushahidi kutoka zaidi ya mashahidi 100 na wapelelezi wa jinai  walipelekwa Rwanda kufanya uchunguzi.

Serikali ya  Rwanda imepongeza uamuzi wa mahakama ya Frankfurt,  kumhukumu Rwabukombe mshukiwa wa mauaji ya Rwanda mwaka 1994.Rwanda inasema hata kama kesi hiyo imesikilizwa nje ya nchi lakini ni ishara kwamba sheria za kimataifa zinaheshimiwa popote pale unapokimbilia.

Kesi ilisikiliza namna kati ya watu 400  hadi  1,200 walivyouwawa hapo April 11 mwaka 1994 kwenye kanisa moja huko Kiziguro, mashariki mwa Rwanda  ambako Rwabukombe wakati huo alikuwa meya.

Mwendesha mashtaka mkuu Christian Ritcher alisema Ujerumani sio mahala pa hifadhi  ya watenda maovu kufuatana na  sheria za kimataifa  anasema huo ndio ujumbe ambao umetolewa jumanne  kwa sauti kubwa  kufuatia hukumu hii.
Rwabukombe alikana mashtaka yote. Mawakili wake wamesema walitaka kesi ifutiliwe mbali na wamesema watakata rufaa.

Kuna baadhi ya nchi  zilizowafungulia mashtaka washukiwa wa Rwanda katika nchi walizokimbilia lakini Kigali  inataka washukiwa walio nje ya nchi kurudishwa nyumbani na kupatiwa hukumu kwenye nchi yao na inasisitiza washukiwa hao kurudishwa nyumbani.

Mataifa mengi yangali yanasita kuchukua hatua hiyo . Watu watano huko Uingereza wanasubiri kesi ya kusafirishwa nyumbani inayotarajiwa kuanza wiki ijayo.

0 comments:

Post a Comment