WATU watatu hawajulikani walipo na wengine 10
wamenusurika kufa, kufuatia chombo walichokuwa wakisafiria kupigwa dhoruba na
kuzama baharini katika maeneo ya Bumbwini wilaya ya Kaskazini 'B' Unguja.
Majeruhi hao wakiwemo ndugu wawili wa familia moja
na raia wawili wa Kenya, walifikishwa hospitali kuu ya Mnazimmoja kwa matibabu
baada ya kuokolewa na wawili kati yao
wanasadikiwa wamekokotwa na maji hadi Bagamoyo.
Akithibitisha tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi
wa mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, SSP Issa Juma Suleiman, alisema, tukio hilo lilitokea majira ya
saa 8:30 mchana wa Februari 14 mwaka huu.
Alisema, ajali hiyo ilitokea wakati watu wapatao
13 wakiwa ndani ya jahazi lijulikanalo kwa jina la Mv Hakim kuzama baharini
baada ya kupigwa na wimbi lililoambatana na upepo.
Alisema taarifa za kuzama chombo hicho
zilipatikana kutoka kwa mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Kheri Juma Nahoda
mkaazi wa Amani.
Alisema, mtu huyo aliielezea polisi wanamaji kuhusu
kuwepo tukio la kuzama kwa jahazi, ndani yake mkiwa na mabaharia 13 na mizigo
ya aina mbali mbali.
Alisema kufuatia ajali hiyo mabaharia wanane
waliogelea na baadae kuokolewa katika maeneo mbali mbali.
Alisema baada ya uokozi huo, majeruhi wanane
walikimbizwa hospitali kwa matibabu na wawili waliokotwa Bagamoyo huku watatu wakiwa
hawajulikani walipo.
Aliwataja majeruhi hao kuwa ni Idd Hassan Hamadi
mkaazi wa Nyerere ambae ndie nahodha wa jahazi hilo, Hamadi Bakari Hassan
mkaazi wa Shumba Mjini kisiwani Pemba na Salum
Bakari Hamadi wa Mtopepo.
Wengine ni Saburi Juma Hija wa Muange Kaskazini
Unguja, Khamis Juma Hija wa Mkwajuni ambao ni ndugu wa familia moja, Juma
Haroub Said anaeishi Mkokotoni na raia wawili wa Kenya Bos Horizoba Okash wa Paje na
Khamis Mohammed Ali.
Waliokuwa hawajulikani walipo ni Hamadi Juma pamoja
na watu wengine wawili waliojulikana kwa majina moja moja la Bakari na Thomas.
0 comments:
Post a Comment