Feb 19, 2014

Mvua, upepo sasa vyaleta maafa




Nyumba zaidi ya 400 zaezuliwa, familia zakosa makazi huku tani 40.6 za chakula zikihitajika haraka huko Mwanga.

Kilwa, Mwanga. Upepo mkali ulioambatana na mvua umesababisha nyumba zaidi ya 150 kuezuliwa pamoja na kubomoa madarasa matano na nyumba za walimu 10.
Wakati mjini Kilwa hali ikiwa hivyo, katika Tarafa ya Ugweno Kilimanjaro jumla ya tani 40.6 za chakula zinahitajika, baada ya mvua iliyoambatana na upepo wa kimbunga kuharibu hekta 262.5 za mashamba na kuezua nyumba 250 na kusababisha watu zaidi ya 800 kukosa makazi.
Mkuu wa Wilaya, Shaibu Ndemanga alimweleza hayo Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe aliyewatembelea wakazi hao kwa ajili ya kutoa pole na kujionea hali halisi ya maafa hayo.
Waziri Maghembe alisema, hali ni mbaya na inahitajika misaada ya haraka ya chakula kunusuru wananchi hao.
Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Abdalla Ulega akizungumzia maafa hayo amesema, baadhi ya wananchi wanahitaji mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kubomoka.
Alisema Kata ya Chumo katika Kijiji cha Nakama nyumba zaidi ya 44, madarasa manane, nyumba ya mwalimu na ofisi zimebomoka, huku katika Kijiji cha Namakolo shule na nyumba ya mwalimu zimeezuliwa.
Ameongeza katika Kijiji cha Mandawa nyumba 78 hazifai baada ya mvua na upepo mkali kuezua nyumba zao, pamoja na ofisi ya kijiji, zahanati, nyumba ya mwalimu, darasa na gulio la kijiji hicho.
Mjini Mwanga mkuu huyo wa wilaya alisema, mbali na msaada wa chakula pia zinahitajika bati 3,762 kwa ajili ya kuezekea nyumba zilizoharibika.
Akizungumza na wananchi waliopata maafa, Waziri Maghembe ambaye pia ni mbunge wa jimbo hilo, alisema kilichotokea katika eneo hilo ni janga na kuwaomba Watanzania wasaidie huku binafsi aliahidi Sh20 milioni.

0 comments:

Post a Comment