Feb 19, 2014

Kificho mwenyekiti wa muda Bunge la Katiba


Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa muda wa Bunge Maalumu la Katiba.
 

Kwa ushindi huo, Kificho atakuwa na kazi kuandaa kanuni ambazo zitatumika kwa ajili ya kumchagua mwenyekiti wa kudumu wa Bunge hilo na kusimamia vikao vyake.

Muda wa mwenyekiti huyo wa muda utamalizika Ijumaa baada ya wajumbe kupitisha kanuni za kuendesha Bunge hilo na kumchagua mwenyekiti na makamu wake.

Akitangaza matokeo hayo, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema Kificho alichaguliwa kwa kura 393 sawa na asilimia 69.13 na kumshinda mpinzani wake Profesa Costa Mahalu aliyepata kura 84 sawa na asilimia 14.79. Kura saba ziliharibika.

Wengine waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ni Magdalena Rwebangira, Sadifa Juma Hamisi na David Mbatia.

Hata hivyo, Mbatia ambaye awali alitambulishwa kuwa ni James Mbatia alienguliwa kutokana na kutokuwa na sifa na Sadifa kujitoa muda mfupi baada ya kujieleza mbele ya wajumbe wa Bunge hilo.

Kabla ya kuanza kwa uchaguzi huo, Dk Kashililah na Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Yahya Khamis Hamad walimteua mmoja wa wajumbe wa Bunge hilo, Oliver Luena kuwa mwenyekiti msimamizi wa uchaguzi huo.

Uchaguzi huo ulioanza saa tisa alasiri hadi saa moja usiku, ulikabiliwa na changamoto kadhaa baada ya upigaji kura kuharibika kutokana na idadi ya wajumbe waliopiga kura kuongezeka kutoka 548 hadi 568 wakati wa kuhesabu.

Hali hiyo ilimlazimu Luena kuagiza uchaguzi huo urudiwe kauli ambayo ilizua mjadala mkali kwa baadhi ya wajumbe kupinga kurudiwa baadhi wakitaka urudiwe na wengine kupinga.

Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde alitaka uchaguzi huo usirudiwe kwa sababu hatua hiyo ingechukua muda mrefu bila sababu za msingi huku Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed akitaka uamuzi huo kufanywa kwa kura.

0 comments:

Post a Comment