Feb 21, 2014

Mtoto aua mama yake kwa jembe

WIMBI la mauaji ya kikatili dhidi ya wanawake limeendela  kutikisa wilaya ya  Kahama mkoa Shinyanga baada ya mwanamke mwingine kushambuliwa na mtoto wake kwa kumkata jembe kichwani wakati akipika chakula cha usiku na kusababisha kifo chake.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Juma Abdalah, tukio hilo lilitokea usiku wa kuamjia jana katika kijiji cha Mwakuhenga kata ya Mwanase wilayani Kahama.

Kamanda Abdalah alimtaja mwanamke aliyeuawa kuwa ni Munde Luchagula mwenye umri kati ya miaka 48 – 50.

Alisema siku  ya tukio wakati Luchagula akiandaa chakula cha usiku ghafla alivamiwa na mwanawe aliyetajwa kwa jina la Mbogo Charles (34) aliyemshambulia kwa kumkata kwa jembe kichwani na kusababisha kifo chake.

Hata hivyo, Kamanda huyo alisema mpaka hivi sasa chanzo cha mauaji hayo bado hakijafahamika japokuwa inahisiwa mtuhumiwa alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya akili.


“Tayari mtuhumiwa tumemkamata, tunaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha kuchukua uamuzi wa kumuua mama yake mzazi, japokuwa inadaiwa anasumbuliwa na ugonjwa wa akili, atapimwa ili kubaini ukweli na baadae tutamfikisha mahakamani kujibu shtaka la mauaji,” alisma.

Tukio hilo la mauaji ni la pili kutokea wilayani Kahama ndani ya wiki moja ambapo tukio la awali lilitokea katika kijiji cha Gula ambako mama na mwanaye waliotambuliwa kwa majina ya Mhulu Nh'ambo (50) na Helena Charles (30) waliuawa kikatili baada ya kushambuliwa kwa kukatwakatwa mapanga na watu wasiojulikana.

 Pia mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka jana wanawake wengine watatu waliuawa kikatili wawili kati yao waliuawa kwa kukatwakatwa mapanga.

0 comments:

Post a Comment