Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), limetangaza Matokeo ya
Mtihani wa Taifa wa kidato cha nne wa 2013, huku ufaulu ukiongezeka kwa
asilimia 15.17.
Matokeo hayo ni ya kwanza tangu kuanza kutumika
kwa mfumo mpya wa upangaji ambao ulipanua wigo wa alama na madaraja,
hivyo kutoa nafasi kubwa zaidi kwa watahiniwa kufaulu.
Licha ya kuanza kutumika kwa mfumo huo, idadi ya
waliofeli imeendelea kuwa kubwa kwani watahiniwa 151,187 sawa na
asilimia 42.91 wamepata sifuri. Kati ya hao, wavulana ni 78,950 sawa na
asilimia 41.54 na wasichana ni 72,237 sawa na asilimia 44.51.
Kadhalika matokeo hayo yameendelea kushuhudia
baadhi ya watahiniwa wakiandika matusi kwenye karatasi zao za majibu,
huku wengine wakichora vitu vya ajabu kwenye mitihani hiyo, huku wengine
wakishindwa kuandika chochote kwenye karatasi hizo.
Akitangaza matokeo hayo jana jijini Dar es Salaam,
Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alisema waliofaulu
mtihani huo ni 235,227 sawa na asilimia 58.25 ya 404,083 ya waliofanya
mtihani huo, ikilinganishwa na 185,940 sawa na asilimia 43.08,
waliofaulu 2012.
Dk Msonde alisema wasichana waliofaulu ni 90,064 sawa na asilimia 55.49 na wavulana ni 111,088 sawa na asilimia 58.45.
Alisema watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani
huo walikuwa ni 427,679 wasichana wakiwa ni 199,123 sawa na asilimia
46.56 na wavulana walikuwa ni 228,556 sawa na asilimia 53.44. Kati yao
watahiniwa wa shule ni 367,163 na watahiniwa wa kujitegemea ni 60,516.
Dk Msonde alisema watahiniwa 23,596 ambao ni sawa na asilimia 5.52 ya waliojiandikisha, hawakufanya mtihani huo.
Dk Msonde alisema matokeo hayo yalipangwa kwa
kutumia alama zilizotangazwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome mwaka jana.
Alama hizo ni A: 75-100, B+:60-74, B:50-59,
C:40-49, D:30-39, E:20-29 na F:0-19. Kabla ya mabadiliko hayo, alama
zilizokuwa zikitumiwa kupanga matokeo ya kidato cha nne ni A:80-100,
B:65-79, C:50-64, D:35-49 na F: 0-34.
Alisema pia alama za maendeleo ya wanafunzi zilizotumika ni 30 huku mtihani wa mwisho ukichangia alama 70.
Kuhusu waliochora na kuandika matusi, Dk Msonde
alisema: “Wengine wamechora nyumba, wengine picha za freemason na
michoro mingine ambayo haiendani na somo husika.”
0 comments:
Post a Comment