Feb 25, 2014

Iran kuwapelekea misaada Waislamu wa CAR

Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran anayeshughulikia masuala ya nchi za Kiarabu na Kiafrika amesema kuwa, hivi karibuni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itatuma shehena ya misaada kwa wakimbizi wa Kiislamu huko Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Akizungumzia radiamali yake kuhusiana na wimbi la machafuko na mauaji dhidi ya Waislamu nchini humo, Amir Hussein Abdullahiyan amesema kuwa, kile kinachoshuhudiwa Jamhuri ya Afrika ya Kati ni matokeo ya siasa chafu na uingiliaji wa baadhi ya madola ya kigeni.

Abdullahiyan ameongeza kuwa, mauaji dhidi ya Waislamu wasio na hatia Jamhuri ya Afrika ya Kati yanatokana na taasubi za kidini za wanamgambo wa Kikristo wa genge la Anti Balaka. 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesema kuwa, kwa miongo kadhaa Waislamu na Wakristo wamekuwa wakiishi kwa amani, lakini madola ya Magharibi yamepandikiza chuki na sumu iliyosababisha kuibuka mauaji ya kinyama dhidi ya Waislamu.

Ameongeza kuwa, Iran inakosoa vikali matendo yanayofanywa na makundi yote yenye kufurutu mipaka ile ya Anti Balaka au Muungano wa Selaka. 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amebainisha kuwa, hivi sasa yameandaliwa mazingira ya kukitokomeza kabisa kizazi cha Waislamu huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, na kusisitiza kwamba kuna ulazima wa kufanyika juhudi maradufu za kuzuia yasitokee mauaji ya kimbari nchini humo, kama yale yaliyojiri nchini Rwanda mwaka 1994.

0 comments:

Post a Comment