Jan 10, 2014

WAFANYABIASHARA WAMJIA JUU MHE KIGODA KUHUSU MASHINE ZA EFD

WAFANYABIASHARA 3,980 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, jana walimuweka kitimoto Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda, wakipinga matumizi ya mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFD.

Mkutano wa Dkt. Kigoda na wafanyabiashara hao, ulifanyika Dar es Salaam jana na kudai mchakato wa kuingizwa kwake nchini haukuwashirikisha kama wadau wa mashine hizo. 


Akitoa msimamo wao , Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wafanyabiashara nchini, Bw. Philimin Chonde ilisema hawakatai kulipa kodi bali wanapingana na Serikali kuhusu matumizi ya mashine hizo kwani hazipo katika mfumo mzuri. 


Alisema mashine hizo zinaonesha zaidi mauzo kuliko faida na hasara ambazo wanazipata hivyo hizo ni kasoro zilizopo katika mfumo wa matumizi yake, ukosefu wa mtandao na haitunzi umeme wa kutosha. 


"Tunakuomba Mheshimiwa Waziri,utufikishie salamu zetu kwa Rais Jakaya Kikwete, tunataka aunde tume huru ambayo itashirikisha wafanyabiashara, wachumi, ofisi ya Rais na washauri wa masuala ya biashara. 


"Tume hii ifanye kazi miezi sita ili kubaini kasoro ambazo zimejitokeza katika mchakato mzima wa utumiaji mashine hizo ili tufikie mwafaka," alisema. 


Bw. Chonde pia alimtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Ernest Mangu, kuhakikisha baadhi ya askari ambao hufanya doria kwa pikipiki mitaani wanaacha tabia ya kuwatisha wafanyabiashara, kuomba na kupokea rushwa hasa baada ya kuingia mashine hizo. 


"Mashine hizi zimeleta ulaji kwa askari polisi, wanashirikiana na Maofisa TRA kutukamata na kututoza kodi kinguvu sawa na mradi wa kufunga vidhibiti mwendo kwenye mabasi," alisema. 


Waliitaka Serikali ikaenao pamoja ili wapeane mbinu za kuongeza ukusanyaji kodi pasipo kutumia mashine hizo ambazo zimekuwa mradi wa watu fulani jambo ambalo linawezekana. 


Akijibu hoja hizo, Dkt. Kigoda alisema amepokea hoja hizo na atazifikisha kwa Rais kwani yeye ni sehemu ya wafanyabiashara hao na mambo yaliyosemwa ni ya msingi kwa mustakabali wa Taifa. 

"Ndugu zangu, kazi yangu ni kuisukuma Serikali iweze kupunguza gharama za biashara kiuchumi hivyo nimechukua maoni yenu nitamfikishia Rais.  "Matatizo ya uchumi yanamalizwa kiuchumi si kidini wala kisiasa hivyo naahidi kuyafanyia kazi matatizo yote," alisema.

Mvutano kati ya Serikali na wafanyabiashara nchini, ulianza baada ya Mamlaka ya Mapato (TRA), kuweka utaratibu mpya wa ukusanyaji wa kodi kwa kutumia mashine za EFD

0 comments:

Post a Comment