Dec 21, 2013

Afikishwa Mahakamani kwa kuoa wanafunzi wawili ndugu

JESHI la Polisi Wilaya ya Nkasi, linamshikilia Pius Jacob, mkazi wa Kijiji cha Chala kwa kosa la kuoa mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya msingi Kabwe, wilayani Nkasi.

Mtuhumiwa huyo pia anadaiwa kumuoa dada wa mwanafunzi huyo ambaye ana miaka 16.

Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Dawati la Jinsia Nkasi, CPL-Anna Kisimba, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya majirani kutoa taarifa polisi kuwa mtuhumiwa anaishi kinyumba na wanafunzi hao.

Alibainisha kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya kumchukua kwa nguvu binti huyo wa darasa la tano mwenye umri miaka 12, na kwenda kuishi naye kama mke na mume.

“Tulikuwa katika ziara zetu za kawaida zilizoambatana na siku 16 za kupinga ukatili tukizunguka baadhi ya vijiji vya wilaya yetu, ndipo raia wema walituarifu kuwepo kwa tukio hilo na kuanza kufuatilia hatimaye kumkamata mtuhumiwa,” alisema Kisimba.

Aliongeza kuwa mtuhumiwa huyo ameshafikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Nkasi, mkoani Rukwa Desemba 10 mwaka huu kwa kosa la kumuoa mwanafunzi na kubaka.

Naye Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri wa Wilaya ya Nkasi, Oscar Mdenye, alisema baada ya kufuatilia zaidi waligundua mke wa kwanza wa mtuhumiwa huyo pia ni mwanafunzi ambaye hata hivyo hakubainisha ni wa shule gani.

Mdenye, alisema majirani waliwaeleza kuwa mtuhumiwa alimpata mwanafunzi wa pili kwa kutumia nguvu na vitisho.

“Hadi polisi na Ofisi ya Ustawi wa Jamii tunafikiwa na taarifa hizo inadaiwa mtuhumiwa huyu alikuwa tayari ameishi na binti huyu wa pili kwa wiki nzima nyumbani kwake, na majirani walijua baada ya binti huyo kulalamika kwao kuwa alikuwa amechukuliwa kwa nguvu na kulazimishwa kuolewa,” alisema Mdenye.

Matukio ya ukatili yanayoripotiwa polisi kupitia Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Nkasi yamekuwa yakipungua ambapo mwaka 2012 kulikuwa na kesi 224 za ukatili zilizoripotiwa ilhali kwa mwaka 2013 ni kesi 143 tu ndizo zilizoripotiwa.

0 comments:

Post a Comment