Nov 19, 2013

SHEIKH PONDA BADO ASOTA

Maombi ya marejeo yaliyowasilishwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda yameshindwa kuanza kusikilizwa jana kutokana na Jaji Rose Temba aliyepaswa kusikiliza kuwa mgonjwa, na sasa shauri hilo litasikilizwa Desemba 2 mwaka huu.
 

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Benard Kongola aliieleza mahakama kuwa wapo tayari kwa ajili ya usikilizwaji wa maombi ya marejeo yaliyowasilishwa na Ponda kupitia wakili wake, Juma Nassoro na kuiomba mahakama iwape siku 21 ili waweze kuwasilisha majibu ya maombi hayo.


Baada ya kutolewa kwa ombi hilo, Wakili wa Sheikh Ponda, Nassoro alidai kuwa yeye hana pingamizi na ombi hilo na kuongeza kuwa muda wa siku 21 ni mrefu kwa kuwasilisha majibu hayo.

“Napendekeza wapewe siku tatu kwa kuzingatia ukweli kuwa maombi yetu waliyapata zaidi ya wiki,” alisema Wakili Nassoro.

Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Projestus Kayoza baada ya kusikiliza maelezo hayo, aliziambia pande zote mbili kuwa Jaji Rose Temba anayesikiliza maombi hayo ni mgonjwa.

Kayoza aliutaka upande wa mashtaka kufaili majibu yao mahakamani hapo, Novemba 25 mwaka huu, kina Sheikh Ponda Novemba 28, mwaka huu na kwamba maombi hayo yatasikilizwa na Jaji Rose Temba Desemba 2.

Sheikh Ponda aliwasilisha maombi hayo ya marejeo kutokana na kutoridhika na uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro wa kukataa ombi lake la kulifuta shtaka la kuwa yeye alivunja masharti ya mahakama la kifungo cha nje.

Kwa mujibu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, jalada la kesi hiyo lilipelekwa Mahakama Kuu tangu Oktoba.

Kesi ilikuwa katika hatua ya kuanza kusikilizwa kwa upande wa mashtaka kupeleka mashahidi wao.

0 comments:

Post a Comment