Oct 18, 2013

Watuhumiwa wa Mafunzo ya Kijeshi waongezeka

WATUHUMIWA 11 waliokamatwa wakifanya mafunzo ya kijeshi yenye asili ya kigaidi msituni katika Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara wameongezeka na kufikia 13,  ambapo kesi yao itaendelea leo katika Mahakama ya Wilaya Nanyumbu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Zelothe Stephen alisema wamekamata watu wengine wawili na kufikia idadi ya watu 13 na kwamba uchunguzi unaendelea kwani kuna mambo mengi yanahitaji uchunguzi wa kina.
Kamanda Stephen alisema watuhumiwa wa awali walikuwa wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Nanyumbu na sasa wanafanya utaratibu ili kesi yao iweze kuhamishiwa Mahakama ya Mkoa wa Mtwara.
“Idadi ya watu waliokamatwa wakifanya mazoezi yenye asili ya kigaidi katika Wilaya ya Nanyumbu kutokana na vifaa walivyokuwa wakitumia sasa imeongezeka na kufikia 13, baada ya kuwakamata wengine wawili,” alisema Stephen.
Kamanda aliongeza kuwa, walitegemea kesi ya watuhumiwa hao ingehamishiwa mahakama ya mkoa, lakini bado kuna taratibu za kisheria ambazo ni lazima zifuatwe na kwamba, wanasheria wapo kwenye mchakato kuona sheria zinazotumika zinatazamwa kwa kina kuona ni nini mashtaka yao.
“Tulitegemea kesi yao ingehamia hapa, lakini  kuna mambo ya kisheria ambayo ni lazima yafuatwe, hivyo tukitoka hapa tunakwenda kumalizia taratibu ili wahamie huku, haya ni mambo ambayo hayaishi kienyeji,” alisema.
Kamanda Stephen alisema vijana hao wanatuhumiwa kwa tuhuma za kupata mafunzo ya kijeshi msituni kwa kutumia CD za Al-Shabaab.

“CD hizo zilikuwa zinatoa mafunzo ya kigaidi ya kundi la Al-Shabaab ya kuchinja watu, mauaji ya Osama Bin Laden, Zindukeni Zanzibar, kuandaa majeshi, mauaji ya Idd Amin na Mogadishu Sniper,” alisema.   

Alisema watuhumiwa wote ni wakazi wa Wilaya ya Nanyumbu mkoani hapa na kwamba, walikuwa wakiongozwa na Mohamed Makande (39), mkazi wa Kijiji cha Sengenya ambaye pia anashikiliwa na jeshi hilo.

Aliwataja wengine waliokamatwa kuwa ni Hassan Omary (39) mkazi wa Kijiji cha Nanyulu, Rashid Ismail (27), Abdallah Hamisi (32), Salum Wadi (38), Fadhili Rajabu (20), Abbas Muhidini (32), Ismail Chande (18), Said Mawazo, Issa Abeid (21), na Ramadhani Issa (26) wote wakazi wa Kijiji cha Likokona.

0 comments:

Post a Comment