Oct 29, 2013

Vijana Tudumishe AMANI-MAHUJAJI


Mahujaji wa Kiislamu waliokuwa wameenda kuhiji Makkah, Saudi Arabia, wamerejea na kuwataka Watazania kudumisha amani.
Mahujaji hao walirejea nchini jana na kulakiwa na ndugu jamaa na marafiki zao katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Walisema, safari yao ilikuwa salama na kwamba wametimiza kwa dhati moja ya nguzo tano za dini. Hajati Mwajuma Adamu kutoka Tanga, alisema amejifunza mambo mengi katika hija hiyo.
Alisema atatumia nafasi hiyo kuwaelimisha vijana kufuata maadili ya dini hiyo kama Mtume Muhammad alivyoelekeza.
“Tunawaomba vijana kudumisha amani, kule tuliishi maisha mazuri katika kipindi chote cha kuwepo kwetu. 

Pia tunawashauri wanaotaka kwenda kuhiji waende wakiwa bado vijana na wasisubiri wakiwa watu wazima kwani kule kunahitajika uwe mwenye afya njema,” alisema hajati Mwajuma.
Alhaj Hamid Rashid wa Dodoma, alisema hija ilikuwa ya mafanikio makubwa hasa ikizingatiwa kuwa iliwashiriki Waislamu wengi kutoka nchi mbalimbali duniani.
Rashid alitumia nafasi hiyo kuwaasa vijana wasisahau kufuata misingi ya dini na kuepuka kujiingiza katika mambo ambayo hayana tija kwao.
Kwa upande wao, Naibu Imam wa Masjid Shafii ya Ilala jijini Dar es Salaam na Kiongozi wa msafara huo, Othuman Zuberi, walisema kati ya mahujaji 18 walioondoka, mmoja ameshindwa kurejea kwa sababu hati yake ya kusafiri imepotea.

0 comments:

Post a Comment