KAMPUNI ya ndege ya FastJet imeahirisha uzinduzi wa safari yake
kutoka Dar es Salaam kuelekea Johannesburg, Afrika Kusini uliokuwa
ufanyike leo, huku ikiahidi kuwarudishia nauli wateja waliokata tiketi
kwa ajili ya safari hiyo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Fastjet, Ed Winter, alisema jana kuwa hali
hiyo inatokana na Mamlaka ya Anga ya Afrika Kusini kuomba kupatiwa
baadhi ya nakala muhimu kutoka Fastjet kabla ya kuanza kutoa huduma
hiyo.
Alisema awali kampuni hiyo ilishakamilisha kila kitu muhimu
kilichotakiwa kufanyika, lakini inashangaza kuona dakika ya mwisho
wanauliziwa nakala nyingine.
Alieleza kwa mujibu wa Mamlaka za Afrika Kusini itachukua siku kadhaa
kuzifanyia kazi taarifa hizo na kutoa kibali hicho kwa kampuni hiyo.
“Hii inakatisha tamaa kwa kuwa hakuna kitu ambacho tulikuwa bado
hatujakamilisha, karibu kila kitu kilikuwa tayari na sisi tulijiandaa
kuzindua ndege yetu hii.
“Kila kitu kikikamilika Fast Jet itaanza kufanya kazi kila Jumatatu,
Jumatano na Ijumaa na kuwa tayari kuongeza huduma zake kadiri mahitaji
ya wateja,” alisema Winter.

0 comments:
Post a Comment