RAIS Jakaya Kikwete ameshangazwa na uongo wa baadhi ya wanasiasa na
hasa madai kuwa Rais aliteua wajumbe wa Tume ya Katiba bila kuongozwa na
mapendekezo ya wadau mbalimbali waliopendekeza majina hayo.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa bado anaendelea kuamini kuwa
mchakato wa Katiba Mpya utafikia mwisho mwa mwaka 2014, na hivyo
kuiwezesha Tanzania kufanya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 chini ya Katiba
Mpya.
Vilevile, Rais Kikwete alisema kuwa hana tatizo na watu wanaopinga
sera za Serikali ama hata kumpinga yeye binafsi bali tatizo lake ni
wanasiasa na wanaharakati wanaochochea ghasia, fujo na uvunjifu wa
amani.
Rais Kikwete aliyasema hayo juzi, mjini San Rafael, California wakati
alipokutana na kuzungumza na jumuia ya Watanzania waishio Jimbo la
California, Marekani, wakati alipoanza ziara yake ya siku mbili katika
jimbo hilo ikiwa ni sehemu ya ziara ya Marekani.
Katika hotuba yake alizungumzia mambo mbalimbali, aligusia mjadala wa
karibuni Bungeni kuhusu mchakato wa Katiba Mpya na kusema kuwa
alishangazwa na madai kuwa yeye kama Rais hakuongozwa na mapendekezo ya
wadau wakati anateua Tume ya Katiba.
“Watu wote niliowateua walipendekezwa na wadau mbalimbali zikiwamo
taasisi za dini. Yule Mama Maria Kashonda alipendekezwa na Baraza la
Maaskofu Tanzania (TEC), Mama Mwantumu Malale alipendekeza Baraza Kuu la
Waislamu Tanzania (Bakwata). Kila kundi ambalo lilipendekeza watu
limepata mjumbe katika tume hiyo wakiwemo walemavu ambao naambiwa
nimewasahau.
“Hivi nyie wanasiasa wenzangu mkikosa hoja mnaongopa hata kwa vitu
ambavyo viko wazi kabisa. Tulikubaliana kuwa Rais angefanya uteuzi wa
wajumbe wa tume baada ya kupokea mapendekezo ya wadau na katika mchakato
ulioendeshwa kwa uwazi kabisa. Hivyo, ndiyo ilivyofanyika.
Sasa uongo
wa nini? Kama hakuna hoja ni kwamba hakuna tu na wala uongo
hautasaidia,” alisema Kikwete.
Kuhusu kama Tanzania itaweza kupata Katiba Mpya kabla ya Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2015, Rais Kikwete amesema: “Ningependa sana, na kwa kweli
ni matarajio yangu makubwa, kuwa tuweze kumaliza mchakato wetu mwaka
2014 na tuweza kuwa na Katiba Mpya ili iongoze Uchaguzi Mkuu wetu wa
mwaka 2015. Mchakato wetu unakwenda vizuri na wala si lazima tuhangaike
na Katiba kwa miaka mingi. Muhimu ni ushirikishwaji wa kila mmojawetu.”
0 comments:
Post a Comment