MWENYEKITI wa Kamati Ndogo ya Mazungumzo kati ya Waislamu na
Serikali, Sheikh Suleiman Kilemile amedai kuwa Mufti Issa Shaban bin
Simba ni msanii katika kupata Mahakama ya Kadhi.
Sheikh Kilemile alisema hatua ya kumuona Mufti Simba msanii imekuja
baada ya kujitokeza akiilaumu Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kupuuza
maoni ya Waislamu ya kutaka kuanzishwa kwa mahakama hiyo.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari na
kuongeza kuwa lawama zilizotolewa na Muft Simba ambaye ni mkuu wa Baraza
Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), zinashangaza.
“Magazeti kadhaa ya hapa nchini Agosti 31, 2013, yamemkariri Mufti
Simba akilalamika kuwa Waislamu wanapuuzwa kuhusu madai yao ya kutaka
Mahakama ya Kadhi hapa nchini.
“Muft Simba ameilaumu Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kupuuza maoni
ya Waislamu ya kutaka kuanzishwa Mahakama ya Kadhi inayotambulika
kikatiba hapa nchini,” alisema Sheikh Kilemile.
Alisema lawama zilizotolewa na Muft Simba zinashangaza kwa sababu
zaidi ya miaka mitatu iliyopita, Rais Jakaya Kikwete alimuagiza Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda awasiliane na Bakwata ili kumtaka Simba aunde jopo
la masheikh kutoka taasisi mbalimbali za Kiislamu ili liwe chombo cha
kuwakilisha Waislamu wote nchini.
“Basi jopo likaundwa kama alivyoagiza waziri mkuu, na hadidu za rejea zikatengenezwa. Kiongozi wa jopo hilo alikuwa Muft Simba.
“Jopo hilo lilikubaliana kwa sauti moja kuwa masuala yote yanayohusu
ufuatiliaji wa Mahakama ya Kadhi hapa nchini yatasimamiwa na jopo hilo
tu na si vyenginevyo,” alisema.
Alifafanua kuwa baada ya kufanyika kwa vikao vingi chini ya uenyekiti
wa Muft na vingine na Pinda mchakato huo ulionesha kufikia hatua nzuri.
Alisema kikao cha mwisho cha jopo hilo chini ya waziri mkuu
kilihudhuriwa na baadhi ya watendaji wa Serikali na mawaziri kadhaa
wakiwemo Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, Waziri wa
Nchi,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) William
Lukuvi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
“Kwa
vile mahakama za kadhi zinapatikana pia katika nchi nyingine za
kisekyula kama Uingereza, India, Kenya na hata Zanzibar, Wassira
alimshauri waziri mkuu upatikane ujumbe utakaokwenda kutembelea nchi
hizo na utakaokusanya wajumbe kutoka serikalini na jopo la masheikh
kujionea taratibu za uendeshaji wa mahakama za kadhi katika nchi hizo
ili utakaporudi nchini uweze kuelekeza jinsi ya kuziendesha mahakama
hizo hapa nchini.
“Pinda alikubali na kuibariki rai hiyo. Aliamuru upande wa jopo la
masheikh utoe wajumbe watatu na upande wa Serikali wajumbe wawili.
Ilikubaliwa kuwa gharama za kupeleka ujumbe huo Uingereza, India, Kenya
na Zanzibar zilipwe na Ofisi ya Waziri Mkuu.
“Ujumbe huo ulitakiwa uwe umekamilisha ziara hizo kabla ya Aprili mwaka huu wa 2013,” alisema.
Sheikh Kilemile alidai kabla ya kufanikisha hayo, Muft Simba alipuuza
yale maazimio ya kikao hicho na badala yake aliamua kuitisha mkutano wa
viongozi wa Bakwata mjini Dodoma na kutangaza jina la kadhi wake mkuu
pamoja na wasaidizi wake bila kushauriana na jopo la masheikh
lililoteuliwa kushughulikia mchakato mzima wa kupatikana Mahakama ya
Kadhi.
“Mtaona alilolifanya Muft Simba ni usanii. Ni kwa sababu hao
makadhi aliowateua hawapo kisheria na wala hawana mamlaka yoyote ya
kiutendaji, kisha Sheikh Simba anathubutu kuinyoshea kidole Tume ya
Mabadiliko ya Katiba na Serikali, eti kwa kuwapuuza Waislamu kuhusu
Mahakama ya Kadhi,” alisema.
0 comments:
Post a Comment