SHEIKH SULEYMAN KILEMILE MWENYEKITI WA HAY-AT
Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu nchini Tanzania umetoa tamko kufuatia kasi ya mashambulizi ya kumwagiwa Tindikali kwa viongozi wa dini yanayoendelea kutokea Visiwani Zanzbar.
Katika tamko hilo lenye kurasa mbili lililo tolewa kwa waandishi wa habari na kusainiwa na Mwenyekiti wa mmoja huo sheikh Suleyman Amran Kilemile,Umoja huo umesema ni "vizuri kwa Watanzania kurejea katika Utamaduni wetu wa kuvumiliana na kushirikiana katika kulinda amani ya nchi yetu".
Aidha tamko hilo lilisema "matukio ya kutumia silaha za moto kama ilivyotokea hivi karibuni ya kuuliwa Padri Mushi kule Zanzibar na kupigwa risasi Sheikh Ponda ni matukio ya hatari na yanaweza kubadili sura nzuri ya Tanzania".
بسم الله الرحمن الرحيم
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Ndugu Wanahabari;
السلام عليكم و رحمة الله,
WATANZANIA TUREJEE KATIKA UTAMADUNI WETU WA
KUVUMILIANA
Sisi Umoja wa Wanazuoni wa
Kiislamu Tanzania
(Hay-atul Ulamaa) tunawasisitizia Watanzania wenzetu kurejea katika utamaduni
wetu tuliokuwa nao karne nyingi zilizopita, utamaduni wa kuvumiana na
kushirikiana katika kuilinda amani hapa nchini.
Kitendo cha Padri wa kanisa
katoliki jimbo kuu la Zanzibar,
Anselmo mwang`amba kumwagiwa tindikali ni kitendo kisichokubalika na ni wajibu
wetu kukilaani kwa nguvu zote.
Hivi ni vitendo vinavyoashiria chuki baina
ya Watanzania wenyewe kwa wenyewe, ambavyo vitakapoachiliwa kuendelea
vitasababisha amani, utulivu, na busara kutoweka nchini.
Si mara chache tena tunasikia matukio kama haya nchini bila ya kumjua muhusika wa dhuluma hizo.
Sheikh Soraga, Sheha Mohammed
Kidevu wa Zanzibar na mfanyabiashara maarufu
Said Saad wa Dar es Salaam
wote hao walikuwa ni wahanga wa tindikali.
Aidha matumizi ya silaha za
moto kama yalivyomuua Padri Mushi, na
kumjeruhi vibaya Katibu wa Jumuiya na Taasisi Sheikh Ponda Issa Ponda.
Matukio kama hayo yote ni
matukio ya hatari ambayo yanaweza kubadili sura nzuri ya Tanzania.
Pia tunachukua nafasi
kuwatahadharisha Viongozi wa dini na wengineo wasikurupuke kuelekeza tuhuma kwa
kikundi dhidi ya kikundi chengine.
Hivyo si halali tukio kama hilo kuhusishwa na udini,
Uzanzibar na wala Utanganyika kabla ya kufanya uchunguzi na kupata dalili
sahihi za kutosheleza.
Mwisho tunaiomba Serikali yetu ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania
kuunda tume maalumu ya kuchunguza matukio haya kwa kina na wahusika wafikishwe
kwenye vyombo vya sheria.
Sheikh Sulaiman A. Kilemile
Mwenyekiti
Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania.
16/09/2013
0 comments:
Post a Comment