Aug 13, 2013

POLISI ALIYEMPIGA RISASI SHEIKH PONDA AKAMATWE-KUNDECHA


  • AITAKA SERIKALI IUNDE TUME HURU.
  • IKIWA NI KWELI,POLISI IMEJENGA MAHUSIANO MABAYA NA WAISLAMU;AL HAD.
  • YASEMWA DAMU YAKE KUWA UKOMBOZI KWA WAPIGANIA HAKI ZA WAISLAMU.
  • WAPIGANIA HAKI HUU SIO UGAIDI?

Na mwandishi wetu wa munira.
Serikali imetakiwa kumkamata polisi aliyempiga risasi katibu wa Baraza Kuu la Taasisi na Jumiya za Kiislamu nchini Sheikh Ponda Issa Ponda ikiwa inazingatia haki na utawala bora.

Hayo yamesemwa na mwenyekiti wa Baraza kuu la Taasisi na Jumuiya za Kiislamu nchini ambaye pia ni Amir wa Shura ya Maimamu Shekh Yusuf Kundecha alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika msikiti wa mtambani.

Amesema tukio la kumpiga risasi Sheikh Ponda ni tukio la kikatiri linalopingana na sheria za haki ya kibinaadamu na haliendi sawa na dhana ya Demokrasia na utawala bora.

"Sisi tunasema tunaitaka serikali hii ikiwa ina sifa ya usikivu basi imkamaete na imfikishe katika vyombo vya sheria askari polisi aliyempiga risasi sheikh ponda bila ya hivyo hatutoilewa serikali".

Aidha alivishukia baadhi ya vyombo vya habari kwa kupotosha habari na kusema hawatendi haki kwani wana wanyima wananchi habari za kweli lakini baya zaidi wanaweza kuiingiza nchi katika matatizo.

Kwa upande wake Sheikh Juma Ramadhan ambaye alikuwa ni mmoja miongoni mwa masheikh waliozungumza na Waislamu waliojazana katika msikiti huo alisema ,"Mtume S.A.W. amesema vitu vitatu viheshimiwe mali za waislamu zisichezewe,heshima ya waislamu isichezewe na damu ya muislamu isimwagwe hovyo,leo katika nchi hii imejengeka tabia ya kumwaga mwaga damu za waislamu,tuna sema damu hii ya Sheikh Ponda ndiyo itakuwa ukombozi katika kupigania haki za waislamu katika nchi hii".

Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake Sheikh wa mkoa wa Dar es salaam Al Had Mussa Salum amesema "ikiwa ni kweli polisi wamempiga risasi Sheikh Ponda,basi itakuwa imefungua mahusiano mabaya na waislamu" na kuongeza kwa kusema wao kama Bakwata haina uadui na Sheikh Ponda japo wana tofautiana katika mawazo.

Kwa upande mwengine waislamu mbalimbali wamejitokeza kutoa maoni yao baada ya kuguswa na tukio la kupigwa risasi Sheikh Ponda ,”alipouwawa Padri kule Zanzibar waziri wa ulinzi na wapigania haki mbalimbal walisema huu ni ugaidi na wakaitwa FBI waje kuchunguza,yalipochomwa moto makanisa wakasema tena kwamba huu ni ugaidi,lilipolipuka bomu kanisani wakasema tena kwamba huu ni ugaidi,lakini hili la kupigwa risasi Sheikh Ponda wote hao wamefunga midomo yao juu ya neno ugaidi,tunakwenda wapi,ina maanisha nini”alisema muumini mmoja kwa uchungu mkubwa.

 
HAWA NI SEHEMU YA WAISLAMU WALIOJAZANA NDANI NA NJE YA MSIKITI WA MTAMBANI KUSIKILIZA TAMKO LA VIONGOZI WA WAISLAMU BAADA YA SHEIKH PONDA ISSA PONDA KUPIGWA RISASI