Mar 7, 2016

WIPA kuendesha mkutano wa kimataifa wa kujadili gesi na mafuta.

Ludovick-Utouh
Taasisi isiyo ya kiserikali ya Wajibu – Institute of Public Accountability (WIPA) imeandaa mkutano wa Kimataifa utakaofanyika kuanzia Aprili 11-12 Mwaka huu, utakaojadili masuala ya uwajibikaji katika sekta ya Gesi asilia na Mafuta.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo Bw.Ludovick Utouh alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambapo lengo la mkutano huo ni kuahakikisha rasilimali ya gesi na mafuta zinainufaisha Watanzania na nchi kwa ujumla.

Utouh ambaye ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Mstaafu, alisema sababu za taasisi-fikra hiyo kuandaa mkutano huo ambao utahusisha wataalam mbalimbali kutoka nje ya nchi watakao wasilisha mada zilizojikita katika masuala ya uwajibikaji ni kujadili na kupata uzoefu wa jinsi kusimamia sekta ya gesi na mafuta.

“Tukiwa kama taasisi yenye lengo la kutoa elimu ya masuala ya uwajibikaji nchini kuwajengea uwezo wataalamu mbalimbali kuhusu dhana ya uwajibikaji, tumeamua kuandaa Mkutano wa Kimataifa utakao lenga sekta ya Gesi asilia na Mafuta ili kupata uzoefu kwa nchi za wenzetu wenye rasilimali hiyo”, alisema Bw. 

Utouh na kuongeza kuwa: “Kwa sasa nchi yetu imegundua sehemu nyingi zenye kiwango kikubwa cha neema ya gesi, hivyo tumeona ipo haja ya kuzingatia masuala ya uwajibikaji na kuifanya rasilimali hii iwe baraka na siyo vinginevyo”,alisema Bw.Utouh.(P.T)

Alisema (WIPA) ina malengo ya kujenga uwelewa mpana wa dhana ya uwajibikaji kwa wananchi na ndiyo maana tumeona ni vyema kuandaa mkutano utakaohusisha wataalamu mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kujadili namna ya kufanikisha suala la uwajibikaji katika sekta Gesi asilia na Mafuta.

Mbali na hayo Mkurugenzi Mtendaji huyo alifafanua kuwa mkutano huo utashirikisha Wakaguzi wa Mahesabu na Wahasibu ambao watasikiliza mada kutoka kwa wataalam wa Kimataifa wa masuala ya uwajibikaji wenye uzoefu wa kusimamia sekta za gesi asilia na mafuta ili kujenga uzoefu wa namna ya kusimamia rasilimali hiyo.

Pamoja na hayo Bw.Utouh alisema Bodi ya Taifa ya Ukaguzi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) itawapa saa 16 ya elimu ya uzoefu wahasibu na wakaguzi wa hesabu watakaoshiriki mkutano huo.

Hata hivyo mkutano huo unaataraijia kuwa na washiriki 100 kutoka Tanzania na 50 kutoka nje ya nchi zenye uzoefu na sekta ya Gesi Asilia na Mafuta na usajili wa kushiriki mkutano huo unafanyika kupitia tovuti ya www.wajibu.or.tz

Baadhi ya watoa mada kwenye mkutano huo ni Bw. Al Kassim, mtaalamu wa Mafuta kutoka Norway, Bw.Lai Yahya kutoka Nigeria, Prof.Patrick Lumumba kutoka Kenya, Mkurugenzi Mtendaji wa TWAWEZA Bw. Aidan Eyakuze, Dkt. Abel Kiyondo kutoka REPOA na Prof. Honest Ngowi kutoka Chuo Kikuu Mzumbe.

0 comments:

Post a Comment