Mar 7, 2016

Misri: Ikhwan/Hamas walimuua mwanasheria mkuu

Misri: Ikhwan/Hamas walimuua mwanasheria mkuu
Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Misri, ameitaja Harakati iliyopigwa marufuku ya Ikhwanul Muslimin na harakati ya mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas kuwa ndio waliohusika katika shambulio la kigaidi dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali ya nchi hiyo.

Magdi Abdul Ghafar amewambia waandishi wa habari kwamba, shambulio dhidi ya Hisham Barakat, mwanasheria mkuu nchini Misri lililojiri mwaka jana lilifanyika katika fremu ya njama kubwa zilizopangwa na viongozi wa Ikhwanul Muslimin kwa kushirikiana na Hamas ya Palestina. 

Aidha amedai kuwa, wanachama wa Ikhwan ndio wahusika wakuu wa hujuma hiyo. Hayo yanajiri katika hali ambayo Jumapili ya jana mwanasheria mkuu wa Misri alitangaza habari ya kutiwa mbaroni watuhumiwa sita wanaohusishwa na mauaji dhidi ya Barakat mwaka jana. 

Kwa mujibu wa habari hiyo, watuhumiwa hao wanaendelea kushikiliwa na jeshi la polisi wakati wakifanyiwa uchunguzi kuhusiana na kadhia hiyo. Hisham Barakat, aliyekuwa na umri wa miaka 64 na mwanasheria mkuu wa Misri aliuawa mwezi Juni mwaka jana akiwa ndani ya gari baada ya kulipukiwa na bomu katika eneo la Heliopolis nchini humo.

0 comments:

Post a Comment