Imechapishwa: Thu, Mar 17th, 2016
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameagiza kufutwa mara moja umiliki wa mashamba makubwa 11 yenye ukubwa wa ekari 7,700 katika vijiji vya Kasharazi na Rwakalemera wilayani Ngara mkoani Kagera.
Mashamba hayo hayana hati na yametelekezwa.
Alitoa agizo hilo jana alipozungumza na wakazi wa vijiji vya Kasulo na Rwakalemera katika Kata ya Kasulo wilayani Ngara akiwa njiani kuelekea mkoa wa Geita.
Waziri Mkuu alilazimika kufanya mkutano huo mapema asubuhi baada ya kuitisha uongozi wa Wilaya ya Ngara ufike kwenye mkutano huo kujibu kero za wananchi waliosimamisha msafara wake wakati akielekea mjini Ngara.
Uamuzi huo ulitokana na hatua ya Waziri Mkuu kumwita kwenye mkutano huo, Ofisa Ardhi na Maliasili wa Wilaya, Betty Munuo aeleze chanzo cha mgogoro wa ardhi katika vijiji hivyo.
Munuo ambaye amehamishiwa wilaya hiyo Agosti mwaka jana, alisema aliyakuta malalamiko hayo na amefanya uchambuzi wa majina ya wamiliki wote wa mashamba na ilikuwa imepangwa wapatiwe notisi wajieleze.
Katika orodha yake, Munuo alitaja wamiliki 18 wa mashamba makubwa lakini kati yao ni wamiliki saba tu ambao mashamba yao yana hati na matatu ndiyo yameendelezwa wakati manne hayajaendelezwa.
Akitangaza uamuzi wake, Waziri Mkuu aliwataja wamiliki wa mashamba yasiyo na hati kuwa ni pamoja na aliyewahi kuwa Katibu Mkuu Utumishi katika serikali ya awamu ya tatu, Joseph Rugumyamheto mwenye shamba na. 527 lenye ekari 505 lililopo Rwakalemera.
Waziri Mkuu aliagiza ifanyike sensa kubaini kama wamiliki wa mashamba hayo yote ni Watanzania au la.
“Haya yenye hati nataka yafanyike mapitio ya hati zao na kubainisha ni namna gani walipatiwa hati hizo.
‘Nataka taarifa inifikie ofisini kwangu Dar es Salaam ifikapo Machi 20, 2016,” alisema.
0 comments:
Post a Comment