Mar 12, 2016

Gavana BoT amjibu Magufuli


Tanzania's President elect Magufuli addresses members of the ruling CCM at the party's sub-head office on Lumumba road in Dar es Salaam
SIKU moja baada ya Rais John Magufuli kueleza kutoridhishwa na mwenendo wa ajira za watumishi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na ulipaji wa malimbikizo ya madeni ya Serikali, Gavana Benno Ndulu ametoa kauli inayojibu hoja zilizoibuliwa na Rais.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana kupitia simu ya kiganjani kuhusu utekelezaji wa hoja na maagizo ya Rais, Gavana Ndulu alisema lipo tatizo la watu kuongea mambo ambayo hawayajui na kwamba hoja na maagizo ya Rais Magufuli anayafanyia kazi.

Juzi Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza BoT ambapo pamoja na mambo mengine alimwagiza Gavana Ndulu kusitisha malipo ya malimbikizo ya madeni ya Serikali yanayofikia Sh bilioni 925 hadi hapo utakapofanyika uhakiki.
Sambamba na agizo hilo, pia alimtaka Gavana Ndulu kupitia upya orodha ya wafanyakazi wa BoT na kuwaondoa wale wote ambao hawana ulazima wa kuwepo katika ajira.
 
Akizungumzia agizo la kuhakikiwa upya kwa malipo ya malimbikizo ya madeni ya Serikali, Gavana Ndulu alisema malipo yaliyotajwa na Rais Magufuli kama malimbikizo siyo hundi bali ni mapendekezo ya wizara na idara mbalimbali za Serikali yanayopitishwa katika bajeti kwa ajili ya matumizi.

“Hakuna fedha zilizorudi Hazina, tatizo watu wanaongea vitu ambavyo hawavijui, hivi ‘exchequer’ mnajua maana yake ni nini? Mnaandika cheque (hundi).

“Zile ni ‘exchequer’ haya ni mapendekezo ambayo wizara na taasisi mbalimbali wanapewa mamlaka ya kutumia. 

 Hutolewa baada ya bajeti na zinapotolewa ile ni ruhusa ya kutumia na si kulipa, unalipa kama zipo fedha, sisi hatuna na kama hamna fedha huwezi kulipa,” alisema Gavana Ndulu.

Alifafanua kuwa taasisi hiyo ambayo ni mhimili mkuu wa uchumi wa taifa, hutoa malipo ya mapendekezo endapo wizara zinazoomba malipo hayo zina fedha katika akaunti zao na si vinginevyo.

“Wao wakipata ruhusa Hazina sisi kama benki lazima tuangalie kama wana fedha za kutumia katika akaunti zao, kama hawana tunaacha. Hata wewe huwezi kwenda benki kutoa fedha wakati akaunti yako haina kitu, hatuwezi kulipa fedha ambazo hatuna,” alisema Gavana Ndulu.

Alisisitiza kuwa hata agizo la Rais Magufuli la kufanya uhakiki wa madeni hayo likitekelezwa na Hazina, bado BoT haiwezi kuidhinisha malipo iwapo mlipwaji hatakuwa na fedha.

Alipoulizwa kuhusu utekelezaji wa agizo la Rais la kupitia upya orodha ya watumishi wa BoT na kuwaondoa wasio na ulazima, alisema hana taarifa za kuwapo kwa watumishi wa aina hiyo.

“Hilo jambo ni la kuniuliza mimi au yeye? (Rais Magufuli), nilisema nitalifanyia kazi na kuhakiki hicho kilichosemwa, yeye amepata taarifa, tutalifanyia kazi ‘unless’ (labda) kama mna ‘information’ (taarifa) mnaweza kutupa. Unaweza kuja hata Jumatatu na ‘document’ (nyaraka) tuzifanyie kazi lakini mimi lazima nilifanyie kazi kwanza maana sina hizo taarifa,” alisema Gavana Ndulu.

Alisema BoT kama taasisi kazi watakayoifanya ni kuhakiki watumishi baada ya hapo ikibainika kuwepo tatizo la aina yoyote watatoa taarifa.

Taarifa zaidi kutoka ndani ya BoT zimeeleza kuwa wakati Rais Magufuli akiagiza kuondolewa kwa wafanyakazi wasiokuwa na ulazima, taasisi hiyo inakabiliwa na upungufu wa watumishi wa kitengo cha utafiti.

BoT ina wafanyakazi 1,391 katika matawi yake sita yaliyopo nchi nzima kwenye mikoa ya Arusha, Mtwara, Dodoma, Mbeya, Mwanza na Zanzibar.

Wakati huo huo, taarifa zilizolifikia MTANZANIA Jumamosi kutoka ndani ya BoT zilieleza kuwa ipo vita ya chini kwa chini inayopiganwa na baadhi ya watumishi waandamizi wa taasisi wanaowania kurithi nafasi ya Gavana Ndulu ambaye anatarajiwa kustaafu kwa mujibu wa sheria wakati wowote kuanzia sasa.

Gavana Ndulu ambaye ana umri wa miaka 66 sasa aliteuliwa kushika wadhifa huo Januari 8, 2008 akichukua nafasi ya marehemu, Daudi Ballali.
chanzo; Mtanzania

0 comments:

Post a Comment