KAMISHNA wa Tume ya
Maadili ya Viongozi wa Utumishi wa Umma, Jaji mstaafu Salome Kaganda,
amesema amewashtaki baadhi ya wateule wa Rais Dkt. John Magufuli katika
nafasi za Mawaziri na Manaibu Mawaziri kwa Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa.
Wateule hao ni wale
ambao hadi sasa hawajajaza fomu za kiapo cha hati ya maadili ya
viongozi kama sheria inavyotaka na kuahidi kumpatia Majaliwa majina ya
viongozi hao.
Jaji Kaganda aliyasema
hayo Dar es Salaam jana katika ufunguzi wa mafunzo maalumu
yaliyoandaliwa na ofisi yake kwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri ili
kuwakumbusha wajibu wa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.
Katika utangulizi wa
hotuba yake mbele ya waziri mkuu alisema kuwa kuna baadhi ya mawaziri na
manaibu wao hadi leo wameshindwa kujaza fomu za kiapo cha maadili ya
utumishi wa umma kwa viongozi wa umma bila kuwepo sababu zozote za
msingi hivyo alibainisha wazi kuwa majina hayo atakabidhi kwa waziri
mkuu.
"Sijajuwa kwanini hadi
leo mawaziri hawa hawakujaza fomu za uadilifu nakuhoji kuwa kama rais
mwenyewe amejaza na hata rais aliyemaliza muda wake alifanya hivi,
sheria inahitaji kila kiongozi wa umma kujaza fomu hizi,"alisema.
Akizungumzia sheria ya
maadili ya utumishi wa umma kwa viongozi alisema kuwa inaelekeza kila
kiongozi wa umma kutangaza mali zake waziwazi hivyo mafunzo hayo
yanalenga kuwaongezea uwezo viongozi wa utumishi wa umma na ili mambo
yaende lazima viongozi wakiwamo mawaziri kuzingatia maadili ya utumishi
wa umma.
Pia Jaji Kaganda
aliwataka mawaziri hao kusoma viapo vyao vya ahadi ya uadilifu na
kuweka katika ofisi zao ili kuweza kukumbuka hususani pindi wanapokuwa
maofisini kwao ili kuepuka kutumia vibaya nafasi zao.
Aidha akizungumzia
changamoto wanazokutana nazo kama Ofisi alisema kuwa tatizo kubwa ni
ufinyu wa rasilimali fedha, vifaa, pamoja na ofisi za kufanyia kazi na
kudai hata wakati mwingine siri mbalimbali za ofisi zinavuja kutokana na
ufinyu wa rasilimali fedha hatua inayosababisha wahisani kutoa fedha
zao ambapo mwisho wa siku na wenyewe wanaingia kwenye vikao muhimu
vyenye maslahi ya taifa.
"Naiomba Serikali
kutuwezesha ili tuweze kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa nakwamba
kukosekana kwa rasilimali fedha kunasababisha tukose hata kufanya kazi
za kiuchunguzi zaidi, lakini tukiwezeshwa tutafanya kazi nzuri
zaidi,"alisema.
Kwa upande wake Waziri
Mkuu Majaliwa akizungumza katika mafunzo hayo yaliyofanyika Ikulu Dar
es Salaam alitoa wito kwa mawaziri na kwa watumishi wa umma na sekta
binafsi kwamba kila mtu kwa nafasi yake atimize ahadi zake na
kuzizingatia na hiyo itasaidia kujenga uwajibikaji, uadilifu na utiifu
katika Serikali wanayoiongoza.
Alisema ni lazima
viongozi wakubali kujenga tabia ya kuzingatia maadili kama heshima
pekee ambayo wananchi wangetamani ionekane kwa kila kiongozi na
mtendaji aliyepewa dhamana, maadili ni tunu ambayo inaweza
kumtofautisha mtu na mtu na yanachochea kujenga tabia ya upendo, umoja
na mshikamano, hali ambayo inaleta maendeleo katika taifa.
"Nikweli kwamba
wananchi wanachukia rushwa na ufisadi na wamechoshwa na vitendo hivyo
hawafurahishwi kabisa na vitendo hivi vya rushwa na ufisadi
vinavyoendelea hapa nchini, vitendo ambavyo vinawanyima haki zao na
kuitia hasara ya mamilioni ya fedha Serikali, fedha ambazo zingeweza
kutumika kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo yao,"alisema
Majaliwa.
Nakuongeza "tatizo hilo
linaweza kutoweka ama kupungua kama tutazingatia sheria ya maadili kwa
ujumla wake na kama tutaweka kipaumbele na umuhimu unaostahili wa
kupambana na rushwa na ufisadi katika nchi yetu,"alisisitiza.
Pia aliongeza kuwa Rais
Dkt. Magufuli katika hotuba yake ya kuzindua bunge mjini Dodoma
alisisitiza kuhusu mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi ambavyo tiba
yake kuu ni uzingatiaji wa sheria ya maadili katika nyanja zote.
Majaliwa pia
alibainisha maeneo ambayo Rais Magufuli aliyaita kero kwa wananchi muda
wote wakati wa kampeni za uchaguzi kuwa ni pamoja na ucheleweshaji wa
utoaji huduma, upendeleo, ubinafsi, rushwa na ufisadi, pamoja na
matumizi mabaya ya madaraka.
"Binafsi Februari, 2016
nilikabidhiwa rasmi hati ya uadilifu ambayo nadhani ni ile baadhi ya
waandishi waliita "Integrity Pledge" ambayo nilisaini hapo awali ambapo
mengi yaliyopo katika hati ile nadhani yanashabihiana, naamini kuwa kila
mmoja wetu aki tekeleza kwa vitendo ahadi zile na kiapo kile tutakuwa
tunatimiza nadhiri yetu kwa wananchi waliotuchagua,"alisema Majaliwa.
Aliongeza kuwa sheria
ya maadili imeweka masharti maalum kwa mawaziri, naibu mawaziri na wakuu
wa mikoa ambapo katika sehemu ya nne kifungu cha 16,17 cha sheria hiyo
kimeweka masharti ya ziada na ambayo yamezingatia katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania (1977).
Alisema katika kifungu
cha 17 kinasema kuwa waziri hatakiwi kufanya jambo lolote linalopingana
na dhana na uwajibikaji wapamoja wa mawaziri kuhusu sera ya serikali na
uendeshaji wa shughuli zake na hataruhusiwa kupinga hadharani au
kujiondoa yeye binafsi katika maamuzi yoyote yanayofanywa na baraza la
mawaziri.
Kutoa hadharani matusi
ya kumkosoa kiongozi mwenzake mwenye madaraka ya uwaziri na kutoa nje
taarifa zisizoruhusiwa za mijadala na maamuzi au nyaraka za baraza la
mawaziri.
0 comments:
Post a Comment