Ukubwa wa vyama viwili vya kisiasa, CCM na CUF uliowagawa wananchi kwenye makundi mawili yanayohasimiana, unafanya suala la maridhiano kabla ya uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar kutokuwa na mbadala, kwa mujibu wa maoni ya wananchi.
Uchaguzi wa rais, wawakilishi na madiwani wa Zanzibar unarudiwa Machi 20 baada ya mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu, akisema kulikuwa na ukiukwaji wa sheria wakati wa upigaji kura na wajumbe wa tume yake kukaribia kushikana mashati.
Jecha alifuta matokeo hayo siku ambayo alitakiwa atangaze mshindi wa kiti cha urais baada ya matokeo ya majimbo 31 kutangazwa na mengine tisa kuwa yamehakikiwa, huku washindi wa nafasi za uwakilishi na udiwani wakiwa wameshatangazwa na kupewa hati za ushindi.
Pamoja na kilio cha wadau kwamba uchaguzi huo usirudiwe hadi hapo pande mbili kuu zitakapofikia mwafaka, ZEC ilisema uchaguzi utafanyika kama ulivyopangwa huku CCM ikiunga mkono na vyama vingine tisa vikitangaza kujitoa.
Akizungumzia msimamo wa CUF na vyama vingine, Katibu wa Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema kususia kwao hakuna athari mbaya Zanzibar kwa kuwa uchaguzi utafanyika kwa amani na utulivu.
“Ukisusa wenzio wala. Wao wamesusa sisi tunasonga mbele. Hatuwezi kuacha kufanya mambo ya maana kwa sababu watu fulani, kwa mtazamo wao, wameamua kujitoa, kususa,” alisema Nape jana.
Lakini, wasomi na wanasiasa waliohojiwa na Mwananchi kuhusu athari za kuendesha uchaguzi uliosusiwa na moja ya vyama vikuu, walisema hakuna shaka kwamba taifa hilo la visiwani litagawanyika kisiasa na kijamii kuzorotesha maendeleo na kurudisha nyuma demokrasia.
Akizungumzia athari za kuendesha uchaguzi uliosusiwa Zanzibar, Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco) alisema iwapo wanachama na wafuasi wa CUF hawatapiga kura, itamaanisha nusu ya Wazanzibar hawatakuwa na rais.
“Impact (athari) ya uchaguzi huo si tu kukosa uhalali, bali kuna uwezekanao mkubwa hata asilimia 50 ya wafuasi wa CCM wasipige kura kutokana na kutokuwa na imani na uchaguzi,” alisema Profesa Mpangala.
“Nyingine ni huyo atakayechaguliwa atakuwa na uhalali wa kisiasa, lakini hatakuwa na uhalali wa kisheria, kitu kinachoweza kusababisha asikubalike sana kimataifa.
Lakini pia asilimia kubwa ya wananchi watakuwa si wazalendo kutokana na kutawaliwa na mtu wasiyemtaka,” alisema.
Profesa Mpangala alisema pia familia zitagawanyika kuanzia Zanzibar hadi Bara na mazingira ya kutawala hayatakuwa na kidemokrasia kwa kuwa kila jambo la Serikali litapingwa.
“Baya zaidi, uwezekano wa kugharimu amani ya nchi ni mkubwa,” alisema.
Msomi huyo alisema baada ya uchaguzi wa marudio, mgogoro wa kisiasa utabaki palepale kwa sababu hautakuwa umepatiwa ufumbuzi.
“Watawala wasilazimishe kutawala kwa mabavu, watafute ufumbuzi wa kudumu kuilinda amani iliyopo,” alisema.
Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe alisema uchaguzi huo wa marudio kufanyika wakati ukiwa umesusiwa hautakuwa halali na utairudisha nyuma Zanzibar. “Kwa sasa uchaguzi hautakuwa na uwezo wa kulinda amani na utaiondoa nchi katika mstari wa maendeleo na kuirudisha nyuma kidemokrasia.
“Hata iweje, itakuwa ngumu kudhibiti nguvu ya vyama hivyo viwili katika uchaguzi kwa kuwa vina wanachama karibu wanaolingana ,” alisema.
Zitto alishauri kutafutwa kwa msuluhishi, asiyekuwa na upande wowote ili kuondoa upendeleo katika kutoa uamuzi, kuundwa kwa jopo la wataalamu litakalorekebisha Katiba na baadhi ya sheria na kuunda tume huru ya uchaguzi.
Profesa Damian Gabagambi wa Chuo Kikuu cha Sokoine (Sua), alisema iwapo suluhisho halitatafutwa kabla ya kurudia uchaguzi, nchi inaelekea kubaya kwa kuwa uadui wa kifamilia utaongezeka na hali ya kiuchumi itazorota kutokana na uwezekano wa mashirika ya kimataifa ya misaada kujitoa.
“Uadui kati ya familia na familia utakuwapo na utadumu kwa miaka mingi kwa sababu wana- CUF wanaamini wanachukuliwa kama watumwa wa kuburuzwa, huku wana- CCM wakionekana wanasikilizwa na kupewa nafasi. Kwa hiyo baada ya uchaguzi huo tension (hali ya wasiwasi) itakuwa kubwa sana,” alisema Profesa Gabagambi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda alikuwa na wasiwasi na ukimya wa CUF.
“CUF wamesusa na kukaa kimya, haijulikani wanajipanga kufanya nini siku ya uchaguzi au baada,” alisema.
Alisema Zanzibar ni kati ya maeneo yenye siasa za kipekee kwa sababu mamlaka ya nchi yanashikiliwa na wananchi.
Alisema kinachosababisha mgongano ni mgawanyo wa madaraka.
“Wakati kuna Serikali ya Umoja wa Kitaifa, licha ya CUF kuwa na wanachama sawa na CCM, bado waliishia kugawana nafasi katika Baraza la Wawakilishi pekee,” alisema. “Hiyo (pekee) haitoshi kwa kuwa wanakuwa hawana meno kamili.
Kutokana na wingi wa wanachama walionao, wanahitaji (kwenye nafasi za) wakuu wa mikoa, wilaya, makatibu wakuu kunakuwa na wanachama wa CUF walio na madaraka,” alisema.
Profesa Abdallah Safari alipendekeza ama kutangazwa kwa Maalim Seif Sharif Hamad kuwa mshindi au kurudi kwenye meza ya mazungumzo.
0 comments:
Post a Comment