Polisi Zanzibar Kuwahoji Watu 34 Wanaotumia Lugha ya Matusi Katika Mitandao ya Kijamii
JESHI la Polisi Zanzibar limetoa tahadhari kwa watumiaji wa mitandao
ya kijamii ambao wanaitumia kwa kuwatukana viongozi wa kitaifa, huku
likiwa na orodha ya watu 34 ambao wanatarajiwa kuhojiwa zaidi kutokana
na matumizi mabaya ya mitandao hiyo.
Kauli hiyo imetolewa juzi na Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai
Zanzibar (DCI), Salum Msangi alipokuwa akizungumza na waandishi wa
habari katika Makao Makuu ya Polisi Zanzibar.
Alisema hivi sasa baadhi ya watu wanaitumia mitandao hiyo kinyume na
maadili jambo ambalo linaweza kusababisha chuki na uhasama na kwamba ni
kinyume na maadili ya wananchi wa Unguja na Pemba.
Msangi alisema jeshi hilo linakusudia kuwahoji watu 34 wanaotumia
mitandao hiyo ya kijamii kwa kuhamasisha vurugu pamoja na kutoa lugha za
matusi kwa viongozi wa Zanzibar, jambo ambalo ni kinyume na sheria
pamoja na utamaduni wa wananchi wa Zanzibar.
Alisema mara baada ya kufutwa kwa uchaguzi Mkuu wa Zanzibar
uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana, kumejitokeza baadhi ya watu na
vikundi mbalimbali vinavyotumia mitandao ya kijamii kwa kuandika maneno
ya matusi au kutoa video za kuzungumza zenye lugha ya matusi kwa
kuwatukana watu mbalimbali hasa viongozi wa kitaifa.
“Tayari orodha ya watu hao imeshapatikana na hadi sasa Polisi
inamshikilia kwa mahojiano na uchunguzi mtu mmoja ambaye anatuhumiwa
kutoa moja ya video hizo zenye lugha ya matusi dhidi ya Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein,” alisema.
Aidha alisema kuwa uchunguzi wa kitaalamu na kisayansi unaendelea na
ukishakamilika jalada litafikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa
ajili ya kulisoma na kulifikisha kwenye hatua zinazofuata.
Msangi alitoa tahadhari kwa wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo
kwani kutumia lugha za matusi ni kosa lililoainishwa kisheria kwenye
sheria ya kanuni ya adhabu, yoyote atakayetenda kitendo hicho atakamatwa
na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria, bila ya kujali limetolewa
mahali gani au wakati gani.
Hata hivyo alisema kuwa wapo watu wanaodhani kuwa demokrasia ni uhuru
wa kuwatukana viongozi, jambo ambalo sio sahihi na halikubaliki
kisheria na kinyume na maadili ya wananchi wa Tanzania ambao wamejengwa
na utamaduni wa kuheshimu watu.
Msangi ambaye pia ni Kamishna Msaidizi wa Polisi Zanzibar, alisema
orodha ya watu wanaojiuhusisha na vitendo hivyo wanayo na wataendelea
kukamatwa mmoja baada ya mwingine na kuchukuliwa hatua zinazofaa kwa
mujibu wa sheria.
Hivi karibuni wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria, Rais wa
Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein alikemea tabia iliyojitokeza sasa ya
matumizi mabaya ya mitandao.
Feb 28, 2016
Jeshi la police laonya kwenye mitandao
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment