Jeshi la Polisi Zanzibar linaendelea kuishikilia kompyuta ndogo (laptop) ya waziri wa zamani wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Mansour Yussuf Himid aliyekamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kupatikana na bunduki na risasi 407 kinyume na sheria.
Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai
Zanzibar, Salum Msangi alisema laptop hiyo iko mikononi mwa polisi tangu
ilipokamatwa Agosti 2, mwaka huu.
Msangi alisema polisi inaendelea kuifanyia upekuzi
ili kujua yaliyomo ndani yake na imehifadhi vitu vya aina gani na iwapo
hakutakuwa na vitu vya uvunjifu wa sheria itarejeshwa kwa mhusika.
Alisema endapo watabaini kuwapo kwa vitu vyovyote
vya uvunjifu wa sheria itatumika kama kielelezo na kwamba kazi ya
kuipekua inaendelea.
“Ni kweli laptop tunaendelea kuifanyia uchunguzi
bado ni mapema kuwaeleza nini tumekiona na hakuna sababu ya kueleza hivi
sasa kwa kuwa kazi hiyo bado haijakamilika,” alisema Msangi.
Hata hivyo, alisema hatua za awali za uchunguzi
zimeonyesha kuna mambo alikuwa akiyatuma kwenye mitandao ya kijamii na
kushiriki hatua mbalimbali za mijadala inayohusu siasa na maendeleo ya
jamii.
Alisema siyo kosa mtu kushiriki na kutoa maoni
katika mitandao ya kijamii lakini kuna mambo zaidi ya hapo yanahitaji
kuchunguzwa.
Mbali na hilo pia walifanya upekuzi katika nyumba
nyingine ya waziri huyo wa zamani iliyopo katika Kijiji cha Kiboje,
kilomita 12 kutoka Mji Mkongwe, Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment