Mjumbe
wa Bunge la Katiba (Chadema) Said Arfi akisaini karatasi ya mahudhurio
bungeni jana, kabla ya kwenda kushiriki mjadala wa kamati yake .
Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe amesema chama chake hakitavumilia vitendo vya usaliti na
kwamba mwanachama yeyote atakayekiuka maagizo ya chama hicho
atachukuliwa hatua kali.
“Katika
hili hatutakuwa na mchezo na naomba niweke wazi kabisa kwamba usaliti
hausameheki.
Tuna vikao vya chama vinakuja siku za karibuni mtu yeyote
ambaye atabainika kusaliti uamuzi wa chama, uwe wa Kamati Kuu au
mwingine wowote, tutachukua hatua hata kama ni kumfukuza uanachama,”
alisema Mbowe.
Mwenyekiti huyo alikuwa akizungumzia taarifa
za kuwapo bungeni, Dodoma kwa baadhi ya wanachama wa Chadema, kinyume
cha makubaliano ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa).
Wabunge hao ni Leticia Nyerere (Viti Maalumu), John
Shibuda (Maswa Mashariki) na Said Arfi (Mpanda Mjini) ambaye aliwasili
jana na kwenda kushiriki kwenye kikao cha kamati namba 10 kilichokuwa
kikifanyika Ukumbi wa Internet, Chuo cha St. Gaspar.
Mbowe
alisema baada ya viongozi wakuu wa Ukawa kukubaliana kwamba
hawatashiriki katika awamu ya pili ya Bunge Maalumu, kila chama
kiliwaelekeza wabunge wake kuhusu msimamo huo ambao pia uliridhiwa na
vikao vya vyama husika.
“Sisi suala hili limepitishwa na
Kamati Kuu ya Chadema, sasa wewe ni nani kukataa, kupinga au kwenda
kinyume cha matakwa ya Kamati Kuu? Ole wake mtu atakayethubutu kushiriki
hivyo vikao vya Kamati za Bunge,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Wakati
tunagombea ubunge 2010 hakukuwa na ahadi kwamba kutakuwa na Bunge la
Katiba, hili limetokea tu, sasa kama sisi kwa masilahi mapana ya umma
tunauona mchakato hauko sawa, kwa nini wewe ulazimishe kushiriki,
unakwenda Dodoma kumwakilisha nani?”
Vyama vingine vyenye
wabunge ambavyo pia wanachama wake wamesusia Bunge Maalumu ni NCCR
Mageuzi na CUF. Kadhalika Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher
Mtikila ni miongoni mwa waliosusia vikao hivyo.
Kauli ya Arfi
Akizungumzia
uamuzi wa kushiriki Bunge alisema licha ya kwamba yeye ni mwanachama wa
Chadema, ameingia bungeni akiwa mwakilishi wa wananchi katika kutunga
Katiba na kwamba ndani ya Bunge hakuna vyama, bali wawakilishi wa
wananchi.
Alisema anaamini katika muungano wa Serikali tatu
na kwamba kama kuna mgongano uliojitokeza lazima uamuliwe ndani ya
mkutano wa Bunge na kwamba kutoka nje ya Bunge ni dalili ya woga na yeye
siyo mwoga.
“Ndiyo nipo kwenye kikao cha kamati namba 10,
hivi sasa hatujamaliza,” alisema Arfi kupitia ujumbe mfupi wa simu yake
ya mkononi baada ya mwandishi wetu kumuuliza jana.
Alipoulizwa
haoni kwamba kufanya hivyo ni kukiuka maelekezo ya chama chake, Arfi
alijibu: “Lakini ipo haki ya uwakilishi, hiyo unaiondoaje? Tutaona
itakavyokuwa.”
Hata hivyo, Shibuda na Nyerere licha ya
kudaiwa kwamba wamesaini kama ishara ya kuripoti katika Bunge Maalumu la
Katiba, hawajaonekana katika vikao vya kamati zinazoendelea.
Shibuda
alisema jana kwamba hakuwapo Dodoma huku kukiwa na taarifa kwamba
Nyerere tayari ameshaondoka kurejea Mwanza tangu juzi jioni baada ya
vyombo vya habari kubaini uwepo wake.
Katibu wa Bunge
Maalumu, Yahya Hamis Hamad alisema jana kwamba wajumbe hao pamoja na
yule wa CUF, Clara Mwatuka hawatalipwa posho yoyote hadi pale Bunge
litakapojiridhisha kwamba wanahudhuria vikao.
“Tulivyofuatilia
attendance (mahudhurio) kwenye kamati, tukakuta kwamba majina yao
hayamo, nikafuatilia fedha asubuhi ya leo (jana) na nikagundua kwamba
hawakuwahi kulipwa na hawakwenda kuchukua,” alisema Hamad.
Hoja ya posho
Mbowe
alisema baadhi ya wajumbe wa Ukawa ambao wamejiandikisha kwamba
wanahudhuria vikao vya Bunge lakini hawaonekani kwenye vikao vya kamati,
wamefuata posho.
“Huo ni wizi maana kama mtu amekwenda
Dodoma halafu akajiandikisha halafu haonekani kwenye vikao, huo ni wizi
wa mchana na mtu wa aina hiyo anapaswa kuchukuliwa hatua,” alisema Mbowe
na kuongeza:
“Wana njaa ya fedha na wanafanya hivyo kwa
sababu wanaogopa kuhukumiwa na umma kwamba wameusaliti. Kwa hiyo wanaona
njia nyepesi ya kupata posho ni kujiandikisha kimyakimya au kwa kificho
halafu walipwe ile posho ya kujikimu”.
Alikiri Sh300,000 ni
nyingi na kwamba wabunge wangependa kupata fedha hizo lakini akasema
mtu yeyote ambaye anaweka mbele masilahi ya posho yake na kuacha misingi
ya kuutetea umma na utaifa, hafai kuwa kiongozi.
“Siyo
kwamba wabunge wetu hawapendi kupata hizo fedha, hapana, lakini
unausalitije umma wa Watanzania kwa sababu ya Sh300,000 kwa siku? Hiyo
ndiyo gharama ya kuwa kiongozi tena anayetetea masilahi ya watu.
Kuhusu
taarifa kwamba baadhi ya wabunge wamekuwa wakionekana Dodoma, Mbowe
alisema lazima ifahamike kwamba mji huo ndiko yaliko makao makuu ya
Bunge la Jamhuri ya Muungano hivyo kuonekana huko siyo dhambi.
“Masuala
mbalimbali ya kiutawala na kihuduma yanafanyika Dodoma, wabunge wana
familia Dodoma na hata ofisi zetu za Kambi ya Upinzani Bungeni zipo
hapo, sasa kama mimi nikiamua kuja kwenye ofisi zangu mtasema kwamba
nimekuja kujadili Katiba?” alihoji Mbowe.
Aug 8, 2014
IDADI YA WASALITI UKAWA YAONGEZEKA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment