Wakati viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakiweka kambi Zanzibar, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta jana naye alitumia siku nzima visiwani humo akikutana na baadhi ya viongozi wa Serikali, katika kile kinachotafsiriwa kuwa kulinusuru Bunge hilo.
Habari zilizopatikana kutoka Zanzibar
zinasema Sitta alikutana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein,
Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, Rais Mstaafu, Aman
Karume na mwanasiasa wa siku nyingi wa CCM, Mzee Hassan Nassor Moyo.
Zanzibar kwa sasa ndiyo moyo wa upatikanaji wa
Katiba Mpya kutokana na wajumbe wake katika Bunge kutegemewa ama
kuipitisha au kuikwamisha kwa kuwa kila upande kati ya mbili
zinazovutana, hauna uhakika wa kupata theluthi mbili za kura.
Baada ya kuondoka bungeni na kutangaza kususia
vikao vya Bunge hilo Aprili 16, mwaka huu, siku mbili baadaye viongozi
wa Ukawa waliingia Zanzibar wakitaka kufanya mikutano ya hadhara
kuwaeleza wananchi sababu za kufanya hivyo, lakini wakazuiwa na polisi
na hadi jana walikuwa wanasubiri kibali.
Safari ya Sitta
Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad pamoja
na kuthibitisha ziara ya Sitta Zanzibar kuwa alikuwa akutane na Dk
Shein, alisema hafahamu lolote kuhusu mkutano wake na Maalim Seif ambaye
pia ni Katibu Mkuu wa CUF.
“Sifahamu malengo ya safari wala walichokwenda
kuzungumza, ila ni kweli kwamba alifika Zanzibar leo (jana) na
alitarajiwa kuondoka jioni kurejea Dodoma,” alisema Hamad na kuongeza:
“Hilo la kuonana na Maalim Seif silifahamu ila
ninachojua aliniambia nimfanyie miadi ya kuonana na Dk Shein na
nikaifanya kama alivyoelekeza.”
Mapema habari zaidi kutoka
Zanzibar zilisema, Sitta baada ya kukutana na Karume, Shein na Mzee Moyo
alitarajiwa kukutana na Maalim Seif saa 9:00 alasiri.
Katibu wa Maalim Seif, Issa Kheri Hussein
alithibitisha kwamba Sitta alikutana na kiongozi huyo nyumbani kwake,
Mbweni saa 9:30 alasiri jana, lakini alidai kutokuwa na taarifa za
mazungumzo hayo.
“Hilo naweza kulithibitisha kwamba mkutano huo
umefanyika lakini mazungumzo yenyewe yalikuwa ya faragha na mimi baada
ya Sitta kufika niliondoka, hivyo sikuweza kufahamu kilichozungumzwa kwa
undani, pengine mpaka nizungumze na Maalim mwenyewe,” alisema Hussein.
Ziara ya Sitta kwenda Zanzibar imekuja wakati
ambao kumekuwa na wasiwasi mkubwa wa kukwama kwa vikao vya Bunge hilo
kutokana na msimamo wa Ukawa.
0 comments:
Post a Comment