JUMUIYA YA KIISLAMU YAUNGANA NA MAASKOFU KUMTETEA WARIOBA
Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania imeungana na maaskofu mbalimbali
kuwataka wajumbe wa Bunge la Katiba kuheshimu Rasimu ya Katiba
iliyowasilishwa kwa mujibu wa sheria na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Pia, taasisi hiyo imemtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Uratibu na Bunge), William Lukuvi kujiuzulu nafasi zake zote za uongozi
kutokana na kauli waliyodai ya kichochezi, aliyoitoa katika Kanisa la
Methodist, Jimbo la Dodoma kuwa ukipitishwa muundo wa serikali tatu,
jeshi litachukua nchi kwa sababu itashindwa kuwalipa mishahara.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Msemaji wa Jumuiya na Taasisi
hizo, Sheikh Rajab Katimba alilaani kauli kuhusu jeshi na kuwa makanisa
yote yatafungwa na nchi itakosa amani kutokana na kupitisha muundo huo
wa serikali.
Sheikh Katimba alisema Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa bungeni na
aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph
Warioba imetokana na utafiti na uchambuzi wa maoni ya wananchi wa
Tanzania Bara na Visiwani ili kuboresha Muungano kutatua kero zilizodumu
kwa miaka 50 sasa.
Msimamo
Jumuiya hiyo iliweka wazi msimamo wake wa kutaka serikali tatu na kutaka
maoni ya makundi mbalimbali ndani ya Bunge la Katiba kuheshimiwa.
Mjumbe wa Jumuiya hiyo, Sheikh Ramadhan Sanze pia alisema si ustaarabu kwa kundi moja kuhodhi mchakato kwa masilahi binafsi.
Alisema kukosoa maoni ya waasisi wa Taifa si dhambi kwa sababu wao
hawakuwa Mungu kwamba hawakosei, badala yake alipendekeza watu waachwe
wazungumze kwa utashi wa matakwa yao juu ya kile kilichowasilishwa na
Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Nchi hii haithamini mchango wa wataalamu, tumeona Tume ilivyofanya kazi
nzuri, leo hii wanatukanwa hadharani, nawashangaa sana viongozi wa nchi
hii,” alisema.
Sheikh Sanze alisema miiko na misingi waliyoiweka waasisi wa Taifa
inavunjwa na viongozi wenyewe ambao leo wanasema waasisi wanatukanwa kwa
kuwa wamependekeza serikali tatu badala ya mbili walizounda waasisi.
“Kulikuwa na utaratibu wa kubadilishana awamu za uongozi katika Serikali
ya Muungano, awamu hii rais akitoka Tanzania Bara, ijayo atatoka
Zanzibar; hii ndiyo misingi waliyoiweka waasisi, mbona leo haifuatwi?
Huu ni unafiki...” alifafanua Sheikh Sanze.
Jumuiya hiyo imewataka wananchi wote kuendelea na mshikamano katika
kutengeneza Katiba Mpya yenye maridhiano na itakayoondoa kero zilizodumu
kwa zaidi ya miaka 50.
0 comments:
Post a Comment