Feb 28, 2014

Viongozi wa Uamsho wapata dhamana Z’bar

uamsho

Viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), wameachiwa kwa dhamana baada ya Jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar, Fatma Hamid Mahmoud kupunguza masharti ya dhamana kutoka fedha taslimu Sh25 milioni kila mshtakiwa hadi kuwa dhamana ya maandishi kwa kiwango hicho.

Uamuzi huo aliutoa jana baada ya wakili wa upande wa utetezi, Salum Tawfiq kuiomba mahakama kupunguza masharti ya dhamana kwa vile wateja wake ni maskini na wameshindwa kukamilisha fedha taslimu, wadhamini watatu kwa sharti lazima wawe watumishi wa Serikali wakati washtakiwa wamefunguliwa kesi hiyo na Serikali.
Wakili Tawfiq aliiomba mahakama iondoe sharti la kuwazuia wateja wake wasitoe mawaidha ya kidini iwe nje au ndani ya misikiti, kwa vile wao ni viongozi wa dini na mawaidha ni sehemu ya ibada hasa kwa siku ya Ijumaa pamoja na kuondoa kizingiti cha kuwazuia kutembea nje ya Kisiwa cha Unguja.

“Mheshimiwa wateja wangu ni maskini, ninapenda kukuarifu kuwa masharti uliyotoa ni magumu kwao na wameshindwa kuyatimiza. Ninaomba yaangaliwe upya kwa vile dhamana ni haki ya mshtakiwa kwa makosa yenye dhamana kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar,”alisema Tawfiq.
Akitoa uamuzi wake, Jaji Fatma alisema kwa mujibu wa Kifungu cha 11(1) cha Katiba ya Zanzibar na Kifungu cha 12(1) kimeeleza kuwa watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki bila ya ubaguzi wowote kulinda na kupata haki sawa mbele ya sheria kwa kuzingatia binadamu wote huzaliwa huru na wote ni sawa.
Alisema kwa msingi huo, amepunguza masharti ya dhamana na kutaka kila mshtakiwa kuweka dhamana ya maandishi kwa kiasi hicho cha fedha Sh25 mil kuwa na mdhamini mmoja ambaye ni mdhamini wa serikali, badala ya watatu na kuwasilisha mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh25 milioni.
Hata hivyo, ombi la kutaka waruhusiwe kutoa mawaidha ndani na nje ya msikiti wakati wakiwa nje kwa dhamana limekataliwa

0 comments:

Post a Comment