Kesi dhidi ya Mchungaji Jean Bosco Uwinkindi anayetuhumiwa kwa mauaji ya
maangamizi nchini Rwanda imeanza mjini Kigali, akiwa mtuhumiwa kwa
kwanza kukabidhiwa Rwanda na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kuhusu
Rwanda.
Uwinkindi anatuhumiwa kwa mauaji ya maangamizi na uhalifu dhidi ya ubinaadamu.
Anasemekana kuwa aliongoza kundi moja la Wahutu katika mauaji hayo ya mwaka 1994 kuwasaka Watutsi. Miili ya watu 2,000 iligunduliwa karibu na kanisa lake. Mwenyewe anakanusha mashitaka yote dhidi yake.
Mnamo mwaka 2001, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kwa ajili ya Rwanda, ICTR, ilitoa waranti ya kukamatwa kwa mchungaji huyo wa zamani na akakamatwa mwaka 2010 nchini Uganda.
Alipelekwa mjini Arusha kwenye makao makuu ya ICTR na mnamo mwezi Aprili 2012 akapelekwa nchini kwake, Rwanda.
Kwa mwanasheria Albert Gasake anayefanyia kazi jumuiya ya SURF inayotetea haki za wahanga wa mauaji hayo ya maangamizi, kesi hii dhidi ya Uwikindi ni ya kihistoria.
"Tunaamini kupelekwa kwa Uwikindi nchini Rwanda kutakuwa pia kutambua maumivu na mapambano ya wahanga wa mauaji hayo kwa ajili ya haki. Uhalifu huo ulitendeka ndani ya Rwanda.
Jamii ya Rwanda sasa inataka kujua kilichotokea mahakamani mbele ya mtuhumiwa." Anasema wakili huyo.
1994 mwaka mbaya kwa Rwanda
Mwaka 1994 ulikuwa mwaka mbaya sana kwenye historia ya Rwanda. Ndani ya kipindi cha siku 100 tu, Wahutu wenye msimamo mkali waliwauwa takribani nusu na robo ya Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani.
Miezi michache baada ya kumalizika kwa mauaji hayo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilianzisha Mahakama Maalum kuhusiana na mauaji hayo mjini Arusha Tanzania.
Kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita, mahakama hiyo imeamua kesi 44 dhidi ya wapangaji na wafanyaji wa mauaji hayo, miongoni mwao wakiwa mawaziri, waandishi wa habari na wanajeshi wa ngazi za juu na watumishi wa umma.
Kesi nyengine 17 bado ziko kwenye hatua ya rufaa hadi sasa, lakini ICTR imemaliza muda wake na inatarajiwa kufungwa rasmi mwishoni mwa mwaka huu.
Ya Kagame hayasemwi
Kwa wawakilishi wa wahanga wa mauaji hayo kama mwanasheria Gasake, ni muhimu kwamba manusura wa mauaji hayo wanapata nafasi ya kushiriki kwenye kesi dhidi ya watuhumiwa, jambo ambalo walishindwa kulifanya wakati kesi hizo zikiendeshwa mjini Arusha.
Gasake anatarajia kuwa wahanga watafidiwa na kwamba Uwikindi atatiwa hatiani nchini mwake.
Lakini si kila mtu anakubaliana na namna kesi za mauaji hayo ya maangamizi zinavyoendeshwa. Mmoja wao ni Gerd Hankel, mtaalamu wa maswala ya Rwanda na mtafiti kwenye Taasisi ya Utafiti wa Kijamii ya Hamburg, ambaye anasema "Mahakama ya ICTR ilifanya kazi kwa kuangalia upande mmoja. Uhalifu uliofanywa na upande mwengine ni mwiko kuusema."
Kwa hili, Hankel anakusudia yale yaliyofanywa na vuguvugu la Rwandese Patriotic Front, RPF, linaloongozwa za Rais Paul Kagame, ambalo liliivamia Rwanda mwaka 1994 na kukomesha mauaji hayo ya maangamizi.
Lakini hadi leo, serikali iliyoundwa na RPF inatuhumiwa kuwa nayo iliendeleza madhila yale yale baada ya kumalizika kwa mauaji ya maangamizi.
0 comments:
Post a Comment