Dec 24, 2013

UMEME WAPANDA BEI


WATANZANIA wataanza Mwaka Mpya 2014 kwa maumivu, baada ya Shirika la Umeme (TANESCO) kuidhinishiwa kupandisha bei za umeme kuanzia Januari mosi.

Uamuzi huo uliotangazwa jana na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), utawalazimu wananchi kulipa zaidi ili wamudu kununua nishati hiyo muhimu katika shughuli za kila siku.

Hivyo, kuanzia Januari mosi mwaka ujao, watumiaji umeme wa majumbani watanunua uniti moja ya umeme kwa Sh 306 kutoka Sh 221 za awali. Wateja wengi wa Tanesco wanaangukia katika kundi hili ambalo linajulikana wateja wa kundi la T-1. Katika kundi hilo ongezeko la bei kwa uniti moja ni Sh 85.

Kundi hilo ni la wateja ambao wanatumia vifaa kama majokofu, televisheni, kupiga pasi pamoja na wafanyabiashara wadogo kama wasusi, vinyozi, maduka, mashine za kusagisha na biashara zingine ndogo zinazotumia umeme.

Katika kundi hilo tozo la kutoa huduma ambayo pia anatozwa mwananchi imeongezeka kutoka Sh 3,841 hadi Sh 5,520 kwa mwezi. Kiasi hicho mteja wa Tanesco anakilipa bila kujali kama ametumia umeme au la kwa mwezi.

Kwa upande wa watumiaji wa majumbani wadogo ambao wamekuwa wakitumia kati ya uniti sifuri hadi 50 ambao wengi wao wanaishi vijijini, watalazimika kununua uniti moja kwa Sh 100 badala ya Sh 60 za sasa.

Katika kundi hilo Ewura imeongeza wigo kuwa sasa kikomo cha watumiaji kitakuwa hadi wateja wanaotumia uniti 75 kutoka uniti 50.

Katika kundi hilo ambalo linajulikana kama D-1 mtumiaji ambaye atavuka matumizi ya uniti 75 kwa mwezi, atalazimika kununua uniti moja ya umeme kwa Sh 350 badala ya Sh 275 za awali. Katika kundi hili hakuna tozo la kutoa huduma kwa mwezi.

Katika mchanganuo kundi la tatu ni T-2 ambako uniti moja ya umeme imepanda kutoka Sh 132 hadi Sh 205. Kundi hilo ni la wateja wenye matumizi ya kawaida ambao hupimwa kwa volti 400 na matumizi ya wastani ni zaidi ya uniti 7,500 kwa mwezi.

Tozo la kutoa huduma kwa mwezi limebaki Sh 14,233. Kundi la T-3-MV ambao ni wateja waliounganishwa katika msongo wa umeme wa kati, bei ya uniti ya umeme itauzwa kwa Sh 163 kutoka Sh 118.

Tozo la kutoa huduma bei yake nayo imepanda katika kundi hilo kutoka Sh 14, 233 hadi Sh 16, 769. Wateja wakubwa ambao wameunganishwa katika msongo wa juu ikiwa ni pamoja na mashirika kama ZECO, Bulyanhulu na viwanda vya saruji kamaTwiga ambao wako kundi la T-3-H, watanunua uniti moja kwa Sh 159 kutoka Sh 106 za awali.

Kundi hilo halitozwi tozo ya kutoa huduma. Gharama za kuunganisha wateja ndani ya meta 30 mijini itakuwa Sh 272,000, vijijini Sh 150,000 na kwa mikoa ya Lindi na Mtwara itakuwa ni Sh 99,000.

Umbali usiozidi meta 70 ambayo mteja ataweka nguzo moja, bei kwa mijini ni Sh 436,964, vijijini Sh 286,220 na umbali usiozidi meta 120 mijini ni Sh 590,398 na vijijini itakuwa Sh 385,300. Ada ya maombi ni Sh 5,000.

Katika eneo la kufunga mita, gharama za kufunga Luku zilizoharibika au kuchezewa na wateja kwa wateja wa kundi la DI na TI bei kwa njia moja ni Sh 60,000, njia tatu Sh 200,000 na njia nne ni Sh 300,000. Bei zote hizo zitadumu kwa miaka mitatu hadi mwaka 2016.


Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi wa Ewura, Felix Ngamlagosi alisema Ewura wamepandisha bei baada ya kubaini kwamba hali ya kifedha ya Tanesco si nzuri, kwani shirika limeendelea kupata hasara ambayo iliongezeka kutoka Sh bilioni 47.3 mwaka 2010 hadi Sh bilioni 223.4 mwishoni mwa 2012.

Alisema pamoja na upungufu kiufanisi, sababu kubwa ya ongezeko la hasara ni kuongezeka kwa gharama za uzalishaji wa umeme ambao Tanesco inanunua kutoka kwa wazalishaji binafsi.

Mara ya mwisho kwa Tanesco kupandisha gharama za umeme ni Januari mwaka jana. “Hali hii imelifanya shirika kushindwa kulipa madeni yake ya muda mfupi na mrefu ambayo yamelimbikizwa hadi Sh bilioni 456.8 ilipofika Novemba, hali ambayo alisema inatishia uendelevu wa huduma ya umeme nchini.

Alisema Ewura imejiridhisha, kwamba ufumbuzi wa matatizo ya kifedha ya Tanesco unahitaji mikakati miwili itekelezwe kwa pamoja ikiwa ni kuongeza bei ya umeme ili kufikia bei inayokidhi gharama halisi, na Tanesco kupata mkopo wa gharama nafuu au ruzuku kutoka serikalini, ili kulipa malimbikizo ya madeni ya shirika.


Ngamlagosi alisema bei hizo zitakuwa zinarekebishwa baada ya miezi mitatu kulingana na mabadiliko ya kiwango na bei za mafuta, mfumuko wa bei, mabadiliko ya thamani ya fedha na upatikanaji ruzuku serikalini.

Alisema Tanesco pia inatakiwa kutekeleza miradi ya uwezekezaji iliyoainishwa kwa kutumia fedha zitakazokusanywa kutokana na bei zilizoidhinishwa.

Alisema Ewura inaweza kurekebisha bei ya umeme kila mwisho wa mwezi 2014 au 2015 endapo Tanesco itashindwa kutekeleza miradi iliyoahidi kutekeleza.

Tanesco inatarajia kutumia Sh bilioni 908.4 mwaka ujao na Sh bilioni 449 mwaka 2015 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya usafirishaji, usambazaji na mingine ili kuboresha huduma.

Kwa upande wa miradi ya kusafirisha umeme, itatumia jumla ya Sh bilioni 54.4 kwa mwaka 2014 na 2015 wakati katika miradi ya usambazaji shirika litatumia Sh trilioni 1.1 huku miradi mingine ikiwamo ya Umeme Vijijini (REA) na umeme wa upepo shirika litatumia Sh bilioni 157.

0 comments:

Post a Comment