Dec 10, 2013

HAMAS yataka Wapalestina kuunganisha nguvu zao

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imewataka Wapalestina kuunganisha nguvu zao kwa shabaha ya kukabiliana na adui Mzayuni. 

Taarifa ya Hamas imebainisha kwamba, Wapalestina wanapaswa kuwa na umoja wa kweli ambao utawasaidia katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imelaani vikali kimya cha jamii ya kimataifa na misimamo ya baadhi ya nchi za Kiarabu kuhusiana na jinai za utawala wa Kizayuni. 

Aidha Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imeitaka Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Arab League kutekeleza majukumu yake ipasavyo kuhusiana na taifa la Palestina. 

Sehemu nyingine ya taarifa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imezitaka OIC na Arab League kuchukua hatua za haraka kuzuia hujuma za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya msikiti wa al-Aqswa na Baytul Muqaddas. 

Vitendo vya Wazayuni vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu navyo vinaripotiwa kushadidi kila leo. Hivi karibuni Mayahudi wenye kufurutu ada waliandika maandishi ya kuutusi Uislamu katika kuta za msikiti mmoja huko Babul Gharbiyah kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

0 comments:

Post a Comment