Nov 28, 2013

Mume Ampa Kilema Mkewe

MFANYABIASHARA, Emmanuel Urio, wa jijini Dar es Salaam amemsababishia ulemavu wa kudumu mkewe, Eva Mollel, baada ya kudaiwa kumsukuma kutoka ghorofani na kusababisha avunjike nyonga, taya na sasa anatembelea magongo.

Tukio hilo limejulikana baada ya Eva kusimulia mkasa huo katika warsha ya kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia iliyofanyika katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) jijini Dar es Salaam.

Akisimulia mkasa huo, Eva mwenye watoto watatu na mume huyo, alisema Agosti 10 mwaka huu alifanyiwa ukatili huo baada ya kumuuliza mumewe kwa nini hakurudi nyumbani jana yake.

“Tarehe tisa mwezi wa nane, mume wangu hakurudi nyumbani, kesho yake nilipomuuliza sababu ya kutorudi alinipiga ngumi ya jicho, akanivunja taya, kisha alinisukuma kutoka ghorofani nikadondoka chini, ilikuwa ni kwenye biashara yetu katika Hoteli ya Temboni Resort,” alisema Eva.
Alisema baada ya tukio hilo, alipoteza fahamu na alipozinduka, alijikuta amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akiwa ametobolewa mguu wa kulia  na kuwekewa vyuma.
 
Alisema alitolewa hospitalini hapo mwanzoni mwa Oktoba baada ya kufanyiwa upasuaji  na kuwekewa vyuma na aliambiwa atakuwa navyo katika maisha yake yote.

Eva ambaye anatembelea magongo hivi sasa, alisema baada ya tukio hilo anaishi kwa kaka yake na alitoa taarifa polisi bila kupata ufumbuzi wa kudumu wa mkasa huo, huku muwewe huyo akiendelea na shughuli zake kama kawaida.

Alisema hilo si tukio lake la kwanza kwani mwaka mwaka 2009, mumewe huyo alimnyoa nywele kwa kisu baada ya kuchelewa kumuandalia supu.  

Pia mwaka 2011 alimuunguza mkono wake wa kushoto na eneo la matiti kwa pasi baada ya kutokea malumbano baina yao.

Vile vile alisema mama mkwe wake 2007 alimng’ata kidole chake cha kati katika mkono wake wa kulia kwa madai kuwa anatembea na mume wake, yaani baba mkwe wake.

Hata hivyo Kaimu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini, Kamishna wa Polisi Isaya Mungulu ambaye alimwakilisha Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema, alisema tukio hilo halitaishia hapo kwani atahakikisha anachukua hatua zinazostahili.

“Jinsi mashuhuda walivyojieleza walivyotendewa na kuripoti polisi bila kuchukuliwa hatua stahili kwa wahusika, iwapo ni kweli hayo yametokea tunakiuka maadili ya kazi yetu. 

Huduma yetu haikuwa nzuri na thabiti, kama kutakuwa na ukweli hatua kali zitachukuliwa,” alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Helen Kijo-Bisimba, alisema walichokifanya katika suala la Eva ni kuwasiliana na polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe, lipo kwenye ngazi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC), lakini kwa kuwa bosi wao amesikia mwenyewe anaamini litafanyiwa kazi kwa haraka zaidi kama alivyoahidi.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa mume wa Eva amegoma kuongea nao na kueleza kuwa waongee na mwanasheria wake.

0 comments:

Post a Comment