RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amemtetea Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kwamba hajakiuka utaratibu wa kuendesha serikali ya umoja wa kitaifa kwa kutoa kauli za kutaka kuwepo mfumo wa Muungano wa serikali tatu na Zanzibar kuwa na mamlaka yake kamili.
Akizungumza Ikulu mjini Zanzibar jana, Dk Shein aliwaambia wandishi wa habari kwamba Maalim Seif hajawahi kutoa kauli ambazo zinahusu msimamo wa serikali kwa mambo mbalimbali na kwamba kama ametoa kauli ni maoni yake binafsi ama ya chama chake.
Dk Shein alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa swali kwamba inakuwaje Maalim Seif anatoa kauli tofauti na msimamo wa serikali hususan mfumo wa Muungano kwa kusema kwamba uwe wa mkataba.
Dk Shein alisema kila mwananchi ana haki kikatiba kufanya jambo analolitaka ukiwamo uhuru wa kutoa maoni:
“Kama Makamu wa Kwanza wa Rais anayo maoni yake kuhusu muundo wa Muungano ni maoni yake au ya chama chake…Lakini siyo msimamo wa serikali…Isitoshe msemaji wa serikali ni mimi labda atoe msimamo wa serikali kwa maelekezo yangu,”.
Aliongeza: “Waziri yeyote wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hawezi kuisemea serikali juu ya Katiba…Mimi sijamsikia (Maalim Seif) anazungumza hivyo kwa niaba ya serikali,” alisema Dk Shein.
Hata hivyo, Dk Shein alisema mawaziri wote wanaounda serikali hiyo wanafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na kwamba hawajawahi kuvutana:
“Tunajadili maslahi ya watu wetu…ukija katika vikao vya Baraza la Mawaziri huwezi kujua nani anatoka chama gani…La msingi ni kuvumiiana na kila mmoja kufuata Katiba,” alisema Dk Shein.
Rais huyo alisema amefanikiwa kuiongoza serikaliya umoja wa kitaifa kwa mafanikio, ingawa alisema kuna wanachama wa CCM ambao wakati inaundwa walimuuliza kama ataweza kuiongoza.
Alipoulizwa kuhusu kutofautiana kwa kauli kati Waziri wa Katiba na Sheria wa Zanzibar, Abubakar Khamis Bakari na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi kuhusu mchakato wa Katiba mpya baada ya Waziri Bakari kusema kuwa Zanzibar haikushirikishwa na Balozi Iddi kusema kuwa ilishirikishwa, Dk Shein hakuwa tayari kujibu hilo na alisema: “Suala hilo limemalizika,”.
Dk Shein aliwashukuru Maalim Seif na Balozi Iddi kwa jitihada na kazi zao kubwa walizofanya katika kipindi cha miaka mitatu kwa kumsaidia kuiongoza Zanzibar: “Umahiri wao na uadilifu wao umesaidia sana katika kuwatumikia wananchi,” alisema Rais wa Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment