Shirika la kutetea haki za binadamu lenye makao yake mjini New York, Human Rights Watch, limesema kuwa ufisadi uliokithiri miongoni mwa maafisa wa Polisi nchini Liberia unahujumu maendeleo ya taifa hilo na kuwanyima raia haki.
Shirika hilo limewashutumu polisi kwa kuwatoza pesa waathiriwa wa uhalifu na kudai mlungula.
Miaka 10 tangu kumalizika vita vya wenyewe kwa wenyewe bado nchi hiyo inasemekana kukumbwa na ghasia na ukosefu wa usalama katika barabara zake.
Na hili halisababishwi tu na wahalifu, ila pia maafisa wanaohusika na kuimarisha usalama. Maafisa wa polisi.
Baada ya kuwahoji zaidi ya waathiriwa 120 wa unyanyasaji wa polisi na ufisadi, shirika la HRW limetoa ripoti inayoshutumu idara ya polisi nchini humo kwa jina , 'Bila pesa, hakuna haki.'
Miongoni mwa mifano iliyotolewa ni waathiriwa kulazimika kulipa pesa kwa polisi ili mashtaka yao yaandikishwe, au kulazimika kulipia gharama ya mafuta ili polisi wafike pahali palipofanyika uhalifu. Pia baadhi wameripoti kuwa washukiwa wanatoa hongo kwa polisi na kuachiliwa kabla ya kufunguliwa mashtaka.
Valerie Brender, ambaye aliongoza utafiti huo anasema kuwa raia wa Liberia wanaogopa kuwasilisha mashtaka yoyote kwa polisi.
"Polisi mara nyingi wanakuwa waporaji kwa raia badala ya kutoa ulinzi na kutetea haki. Wanajihusisha na uhalifu mwingi. Wengine wametaumbia kuwa hao polisi waliojihami ni sawa na wahalifu waliojihami. Yale yanayofanywa na majambazi ni sawa na yale polisi hao wanafanya. Wanawapokonya simu zao, pesa na wakati mwingine hata wanawashambulia kikatili.''
Mkaazi mmoja wa mji wa Monrovia amesema kuwa polisi walimvamia nyumbani kwake na kumpiga mateke. Walimshikia mke wake bunduki na kumlazimisha kutoa pesa alizokuwa ameficha. Waendesha piki piki na madereva wa Taxi pia wameelezea unyanyasaji unaofanywa na polisi wa trafik. Shirika hilo la haki za binadamu limesema kuwa rais Ellen Johnson Sirleaf aliahidi kuunda tume huru ya kiraia itakayochunguza visa hivi vya ufisadi miongoni mwa maafisa wa polisi lakini hadi sasa haijafanyika.
Na huku Kikosi cha umoja wa mataifa cha kuweka amani kikijiandaa kumaliza oparesheni zake nchini Liberia mwaka ujao, wengi wanahofia kuwa nchi hiyo haiko tayari kusimamia usalama wake.