AKUMBUSHIA YA MWAKA 1992.
LICHA ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kutangaza msimamo wa kukataa serikali
tatu, Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, amewataka wake wajiandae
kisaikolojia kwa mabadiliko yoyote yatakayotokea kinyume na matakwa yao.
Kwa mujibu wa chanzo kimoja kutoka ndani ya kikao cha Baraza la Kikatiba la
Halimashauri Kuu ya CCM ambalo linapitia vifungu vya rasimu ya Katiba Mpya,
Rais Kikwete aliwataka makada wenzake kujiandaa kwa lolote kama
ilivyotokea mwaka 1992.
Rais Kikwete alisema mwaka 1992 idadi kubwa ya wanachama wa CCM walikataa
mfumo wa vyama vingi lakini mfumo huo ulipita.
Kiongozi huyo alisema katika kikao hicho cha mwaka 1992 ilikubalika kuwa
‘wengi wapewe wachache wasikilizwe’.
Katika kikao cha jana Kikwete aliwataka wana CCM wajiandae kisaikolojia kwa
jambo lolote litakaloamriwa na wananchi watakaopiga kura juu ya rasimu ya
Katiba mpya.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Dk. Asha Rose
Migiro, aliwasilisha na kuchambua upungufu uliopo kwenye rasimu ya Katiba Mpya
iliyotolewa hivi karibuni na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kutokana na upungufu huo hasa katika mfumo wa serikali idadi kubwa ya makada
wa chama hicho ilikubaliana kuendelea na msimamo wao wa serikali mbili.
Mara baada ya Migiro kumaliza, walisimama wajumbe kadhaa na Kikwete kumpa
nafasi mmoja wao ambaye alitaka wasiendelee na suala la Katiba mpya liahirishwe
mpaka baada ya mwaka 2015.
Inaelezwa kuwa mjumbe huyo kutoka Zanzibar,
alijenga hoja kuwa suala la Katiba mpya halikuwa kwenye ilani ya uchaguzi wa
chama hicho ya mwaka 2010.
Mjumbe huyo alisema ilani ya chama hicho ilitoa ahadi za ujenzi wa madaraja,
barabara, ununuaji wa meli na nyinginezo nyingi ambazo mpaka sasa bado.
Alisema ni busara CCM ikaachana na hoja hiyo mpaka baada ya uchaguzi wa
mwaka 2015.
Hata hivyo baada ya mjumbe huyo kutoa hoja hiyo, Kikwete aliwataka wajumbe
wajadili mantiki ya rasimu ya Katiba mpya badala ya kufoka au kubishana.
Rais Kikwete alisema mazingira ndiyo huamua jambo fulani hivyo hakuna sababu
hoja hiyo ya Katiba kutojadiliwa hivi sasa.
Inaelezwa kuwa Rais alisema licha ya asilimia 80 ya Watanzania kutoukubali
mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 hoja hiyo ilipita kutokana na mazingira.
Alisema licha ya hofu ya Watanzania juu ya mfumo wa vyama vingi bado mfumo
huo umendelea kuwepo mpaka hivi sasa na umeonyesha maendeleo.
Baada ya kauli hiyo wajumbe walianza kupitia kifungu kwa kifungu Rasimu ya
Katiba mpya ambapo wengi walipinga muundo wa serikali tatu uliopendekezwa na
Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Msimamo wa CCM
Chama hicho tawala tangu kutoka kwa Rasimu ya Katiba kimekuwa kikisisitiza
msimamo wa kutambua serikali mbili na si tatu kama
ilivyotolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph
Warioba.
Kamati Kuu (CC) iliyoketi Juni mwaka huu iliamua kuipeleka rasimu hiyo kwa
wananchi wake kuanzia ngazi ya matawi na kutaka yaundwe mabaraza ya Katiba ya
chama hicho.
Hata hivyo CCM ilishaweka wazi msimamo wake kuwa haitokubali muundo wa
serikali tatu.