Aug 8, 2014

UVAMIZI WAMPONZA MCHUNGAJI,ABOMOLEWA NYUMBA ZAKE

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Makazi jana imebomoa nyumba nne zilizojengwa ndani ya kiwanja namba 314 zilichopo eneo la Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam zinazomilikiwa na Mchungaji Getrude Rwakatare kwa tuhuma kuwa alivamia eneo hilo.

Kazi hiyo ya ubomoaji, ilitekelezwa chini ya ulinzi mkali wa Polisi na iliendeshwa kwa pamoja na maofisa wa Ardhi kutoka wizarani na Manispaa ya Kinondoni, waliodai wamepewa agizo hilo na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Alphayo Kidata.

Mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni, Baraka Mkuya alidai wamepewa agizo na Katibu huyo, kuvunja nyumba ndani ya kiwanja hicho, baada ya kubainika kuwa eneo hilo siyo mali ya Rwakatare, hivyo hastahili kujenga mahali hapo.

Mhandisi Mkuya alidai pamoja kutokuwa mmiliki halali wa eneo hilo, nyumba hizo pia zimejengwa bila utaratibu, ikiwemo kupata kibali cha ujenzi kutoka katika manispaa hiyo, suala linaloashiria kuwa kulikuwa na kitu kimejificha.

“Sisi kama manispaa tumekuja kutekeleza agizo la kubomoa kutoka kwa Katibu Mkuu, kinachoonyesha ni kuwa aliyejenga eneo hili alivamia eneo la mtu mwingine huku akijua wazi ni kinyume cha utaratibu” alidai Mkuya.

Alidai matatizo ya uvamizi wa viwanja, yamekuwa ni jambo la kawaida hasa katika Manispaa ya Kinondoni na kwamba wanaendelea kuyashughulikia kwa lengo la kuyapatia ufumbuzi wa haraka.

Awali, kazi hiyo ya ubomoaji ilitanguliwa na ‘vuta nikuvute’ baina ya mwanasheria aliyedai kuwa anamwakilisha Rwakatare, Emmanumuel Muganyizi na Mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni, Baraka Mkuya kuhusu suala la kubomolewa kwa nyumba hizo, zinazodaiwa kujengwa ndani ya kipindi kisichozidi miezi miwili na kupauliwa kwa vigae.

Huku akiwa na nyaraka mbalimbali za kesi, alidai kesi bado ipo katika Mahakama ya Kinondoni. Muganyizi alisema anashangazwa na uamuzi huo uliochukuliwa kwa madai kuwa suala hilo, halijapatiwa ufumbuzi wa kisheria na Mahakama.

“Ninaamini hiki kinachoendelea hapa ni sawa na uvunjifu wa amani, kesi bado ipo mahakamani inapaswa iachwe iishe ndiyo uamuzi ufanyike. Kwa hili mnalofanya sasa siyo sawa kabisa,” alisema Muganyizi.

Mwanasheria huyo wa Rwakatare, awali aliingia katika mzozo na waandishi, akidai kushangazwa na kitendo chao cha kutaka kuandika habari hiyo.

Alidai habari hiyo haina manufaa kwa jamii, kwa kuwa inahusu madai ya mtu na mtu. Kwa upande wake, mtu anayedai kuwa mmiliki wa kiwanja hicho, aliyekuwepo wakati kazi ya uboaji ikiendelea, Janeth Kiwia, alidai kiwanja chake kilivamiwa na kuanza kujengwa mwishoni mwa mwaka jana wakati akiwa safarini kwa watoto wake nje ya nchi.

Alidai kabla ya kuvamia eneo hilo, kulikuwa na nyumba ya vyumba vinne, aliyokuwa akiijenga taratibu, ambayo hata hivyo ilibomolewa na msingi wake kutumika kujenga moja ya nyumba hizo.

“Tayari kulikuwa na nyumba iliyokuwa imefikia usawa wa rinta, lakini cha kushangaza walipovamia waliibomoa na kujenga ya kwao, namshukuru Mungu kwa kuwa haki imetendeka baada ya kuhangaika huku na kule kutafuta haki yangu,” alidai Janeth.

Alidai kitendo hicho, kimemfanya kujenga imani na Serikali kuwa inatenda haki, bila kujali kuwa aliyekuwa akiporwa na mnyonge, huku akiitaka kuwasafisha baadhi ya watendaji waliopo ndani ya wizara hiyo, wanaoshirikiana na watu wabaya kutaka kupora haki za watu.

“Nilikuwa sitarajii kama ningefanikiwa tena kupata kiwanja changu, namshukuru Mungu haki imetendeka bila hata mimi kutoa Shilingi moja, naomba tusife moyo na Serikali yetu kwa kuwa inafanya kazi,” alisisitiza Janeth.

0 comments:

Post a Comment