Aug 17, 2014

Mwinyi awaonya wanaotoa mawaidha potofu ya dini

 
Wanazuoni wa Dini ya Kiislamu wakifuatilia mawaidha yaliyokuwa yakitolewa na wakufunzi mbalimbali kwenye semina ya kutoa elimu ya dini Dar es Salaam jana.

Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi amekemea mawaidha potofu yanayotolewa na baadhi ya wanazuoni wakiwataka Waislamu nchini kutofundishwa elimu dunia.

Mwinyi alitoa rai hiyo jana, kwenye Kongamano la Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, lililoandaliwa na Chuo cha Kiislamu cha Kimisri cha Al-Azhar Shariif, ambalo lilijadili mauaji kinyume cha Sheria za Kiislamu.
“Elimu ni suala nyeti, tukemee uondoaji wa watoto wa Kiislamu shuleni na vyuoni kwa uongo kwamba ni elimu ya kikafiri,” alisema Mwinyi. Aliongeza: “Nastaajabu yanayotendeka Kigoma, hata yanayofanywa na Boko Haram kwa jina la Uislamu. 

Uislamu haupiganiwi kwa kuteka, kunajisi, kuua wala kuwalazimisha wasiokuwa tayari kuufuata.”
Alhaji Mwinyi alijumuika na masheikh pamoja na wanazuoni wa hapa nchini na Misri kujadili mwenendo wa mauaji yanayoendelea katika sehemu mbalimbali duniani yakifanywa chini ya mwamvuli wa Uislamu ambapo walieleza kuwa kila kiumbe kina haki ya kuishi.
“Kuna taarifa tumezipata kuwa kuna masheikh kutoka Oman walikwenda Kigoma na kuwaagiza Waislamu wawaondoe watoto wao shuleni au vyuoni ili wasipate elimu dunia.
Viongozi wa Uislamu tupige kelele kwa kuchukua hatua thabiti kuiokoa dini yetu kwani Boko Haram walianza kama hivi lakini hakuna aliyewajali wa kidhani kuwa hakuna atakayewazingatia na kuwasikiliza na sasa wanaleta machafuko Nigeria,” alisema Sheikh Mataka.
Naye Sheikh Suleiman Kilemile kutoka Tandika wilayani Temeke, alieleza kuwa viongozi wa dini wanapaswa kusimamia misingi ya dini hiyo ipasavyo ili kuzuia watu wanaotumia nyumba za ibada kutoa hisia zao binafsi akisema huko siyo sehemu sahihi.
Naye Sheikh Salah Sayed Hussein Maftaha, raia wa Misri ambaye pia ni mkuu wa chuo hicho, alisema kuwa wameandaa kongamano hilo ili kuwapa Waislamu wa Tanzania na Misri fursa ya kujadili na kulaani upotoshaji wa maadili ya dini unaofanywa sehemu mbalimbali duniani.

0 comments:

Post a Comment