Aug 13, 2014

Abbas ataka Netanyahu afunguliwe mashtaka ICC

Mahmoud Abbas  
 Mahmoud Abbas 
 
Mahmoud Abbas Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameitaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kumfungulia mashtaka Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kutenda jinai za kivita na kufanya mauaji ya halaiki dhidi ya wananchi wa Ghaza.
Matamshi ya Mahmoud Abbas yanatolewa katika hali ambayo, Umoja wa Mataifa kupitia Baraza la Haki za Binadamu la umoja huo umeshaunda tume huru ya kuchunguza vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu na jinai za kivita vilivyofanywa na majeshi ya Israel dhidi ya Wapalestina wa Ghaza.

Wakati huohuo, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Israel amesema kuwa, utawala huo hautashirikiana na tume huru ya Umoja wa Mataifa ya kuchunguza jinai zilizofanywa na Wazayuni huko Ghaza. 

Avigdor Lieberman ameituhumu tume hiyo ya Umoja wa Mataifa kwamba haitafanya uadilifu katika utendaji wake na kusisitiza kwamba, kamwe Israel haitaitambua rasmi tume hiyo.

Kwa upande mwingine, Avigdor Lieberman ametishia kuwauwa viongozi waandamizi wa Hamas akiwemo Ismail Haniya Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas na Muhammad Deif Makamanda wa tawi la kijeshi la Hamas, iwapo harakati hiyo haitawaachilia huru wanajeshi wawili wa Israel waliotekwa na wanamagambo wa Kipalestina.

Inafaa kuashiria hapa kuwa, kwenye mashambulio yaliyochukua muda wa siku 36 ya majeshi ya Israel dhidi ya wananchi wa Ukanda wa Ghaza, kwa akali Wapalestina 1,960 wameuawa shahidi wengi wao wakiwa wanawake na watoto na wengine 10,000 wamejeruhiwa.

0 comments:

Post a Comment