Mar 1, 2014

Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran alaani mauaji ya Waislamu CAR

Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami
Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya Tehran amekosoa vikali kimya cha jamii ya kimataifa mbele ya mauaji ya umati yanayofanyika katika Jamhuri ya Afrika ya Kati dhidi ya Waislamu. 

Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami amebainisha masikitiko yake kuwa makundi ya Wakristo wenye misimamo mikali wameachwa kuendelea na mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu katika nchi hiyo ya Kiafrika. Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran ametoa mfano wa namna Waislamu 70 wakiwemo wanawake na watoto walivyouawa katika kijiji kimoja huko Jamhuri ya Afrika ya Kati. Amesema kama ambavyo taasisi za kimataifa zimeonya, iwapo hatua hazitachukuliwa, basi hakutabakia Mwislamu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Ayatullah Khatami amesema mauaji ya Waislamu katika nchi hiyo ya Kiafrika ni sehemu ya wimbi la chuki dhidi ya Uislamu duniani, chuki ambazo amesema zinaenezwa na madola ya kibeberu na kiistikbari.
Ameongeza kuwa chuki hizo zinatokana na kuibuka wimbi kubwa la kuenea Uislamu duniani.

 Ayatullah Khatami ameongeza kuwa, Uislamu halisi wa Mtume Muhammad SAW ni nguvu kubwa mbele ya madola ya kibeberu na utawala wa Kizayuni.

 Aidha amesema kuwa hivi sasa Iran ni makao ya Uislamu huo halisi na hii ndio sababu maadui wanaiogopa Iran.

Ayatullah Khatami ameendelea kusema kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel ndiye adui anayechukiwa zaidi na Waislamu.

 Ayatullah Khatami amesema Marekani inataka Uislamu wa Kimarekani ambao unafuatwa na watawala wa nchi za Kiarabu kwani ni kwa maslahi ya malengo yake haramu. 

 Aidha amekosoa vikali Marekani na Saudi Arabia kwa kuwatumia silaha magaidi nchini Syria na kusema kwa hatua yao hiyo, wanachochea mauaji ya Waislamu wa Syria.

Khatibu wa Sala ya Ijumaa pia ameulaani vikali utawala wa Aal Khalifa nchini Bahrain kwa kuendelea kuwaua Waislamu wanaoandamana kwa amani nchini humo. 

Kwingineko katika hotuba yake Ayatullah Khatami amesema vikwazo vyote vya upande mmoja vya nchi za Magharibi dhidi ya Iran vitasambratatishwa kupitia 'uchumi wa kusimama kidete'. 

Ayatullah Khatami ameongeza kuwa, uchumi wa kusimama kidete ni hatua kuelekea katika uhuru kamili wa kiuchumi nchini Iran na hivyo kuondoa kabisa utegemezi wa kigeni. 

Ameendelea kusema kuwa uchumi wa kusimama kidete unategemea ujuzi, elimu na teknolojia ya ndani ya nchi  na uadilifu. 

Ameendelea kusema kuwa kwa kutegemea mamilioni ya wataalamu Wairani, miundo msingi iliyopo na utajiri mkubwa wa mafuta na gesi, Iran inaweza kufanikiwa katika sera ya 'uchumi wa kusimama kidete'.

0 comments:

Post a Comment