Maamkizi Ya Kiislam 'Assalaamu 'Alaykum' – Amri Na Fadhila Zake - 1
1 - Umuhimu Wake
Kutoa
salaam ni funzo muhimu tulilofundishwa na kuamrishwa katika Dini yetu,
lakini tunaona kwamba limechukuliwa kuwa ni jambo jepesi lisilotiliwa
hima na ilhali lina fadhila kubwa sana, na mojawapo ni kumfikisha mtu
katika makazi ya Peponi.
عن أبـي هريرة رضي الله عنه قال: قال رسول الله : «لا تَدْخُـلُوا الـجَنَّةَ حتـى تُؤمِنُوا، ولا تُؤمِنُوا حتـى تَـحابُّوا أوَلا أدُلُّكُمْ علـى شَيءٍ إذا فَعَلْتُـمُوهُ تَـحَابَبْتُـمْ؟ افْشُوا السّلامَ بَـيْنَكُمْ»". صحيح مسلـم
Kutoka
kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hamtoingia Peponi hadi muamini,
na wala hamuwezi kuamini hadi mpendane. Je, nikujulisheni jambo ambalo
mtakapolifanya mtapendana? Toleaneni Salaam baina yenu)) [Muslim]
Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipohamia Madiynah,
mafunzo ya maamkizi ya salaam yalikuwa ni katika mafunzo ya mwanzo
kabisa kuwapa Maswahaba alipoyatoa katika khutba zake za mwanzo huko.
Mafunzo haya pia yanabainisha kuwa kuamkia kwa maamkizi ya Kiislamu ni
jambo litakalomuingiza Muislamu katika makaazi ya Pepo:
((ايها الناس ،أفشوا السلام، وأطعموا الطعام، وصلّوا بالليل والناس نيام تدخلوا الجنة بسلام)) رواه الترمذي، حديث صحيح
((Enyi
watu, toeni (amkianeni kwa) salaam, na lisheni chakula, na Swalini watu
wanapolala (Tahajjud), mtaingia Peponi kwa amani)) [At-Tirmidhiy – Hadiyth Hasan]
Waislamu
wanapokutana au kuwasiliana kwa njia yoyote inawapasa kusalimiana kwa
maamkizi ya Kiislamu kama tulivyoamrishwa, yaani kuanza angalau kwa
"Assalaamu 'Alaykum". Lakini inasikitisha kwamba wengi wetu hatufuati
amri hii. Sababu ni ima usahaulifu au wengine hupatwa na aina ya kiburi
na kuhisi kwa nini awe yeye kila siku tu anayeanza? Wengine huanza na
"Hujambo? "Habari gani?" "Hali?" "Vipi mzima?" "Habari za asubuhi" au
'Swabaahal-khayr" "Ahlan" "Marhaba". Na kuna salaam nyinginezo
zilizoenea katika jamii yetu zisizo hata na maana kama ‘Shikamoo’ na
anayesalimiwa hujibu ‘Marahaba’, na tena salaam hiyo ina sharti; huwa ni
ya upande mmoja kuanza kusalimia; mdogo kumsalimia mkubwa! Na wengine
ni sababu ya uvivu kwani hufupisha maamkizi haya katika mawasiliano ya
barua, maandikiano ya simu za mkononi (text messages) ambayo ndio
yameenea sana katika zama zetu hizi, barua pepe (e-mail) kwa kuandika
ima A.A, au A.A.W, au A.A.W.W.B. Wamekosa kutambua kwamba wanakosa
fadhila kubwa za kuamikiana kikamilifu, jambo ambalo halimchukui mtu
hata dakika moja kuandika kirefu 'Assalaamu 'Alaykum' au Assalaamu
'Alaykum wa RahmatuLLaahi wa Barakaatuh'.
Lakini
bila ya shaka hayo ni kutokana na kukosa mafunzo haya muhimu na
kutokutambua fadhila zake. Kwa hiyo tumeona kwamba ni jambo muhimu
kupeana mafunzo haya na kukumbushana kwa umuhimu wake kwa vile
tunapambana nayo kila siku, kila wakati katika maisha yetu katika
mawasiliano baina yetu. Tunatumai kwamba baada ya kuzijua fadhila zake
zifuatazo hapa chini, kila mmoja wetu atakimbilia kuanza yeye kutoa
maamkizi yetu ya Kiislamu yaani kusema: 'Assalaamu 'alaykum'.
Zifuatazo ni Aayah na Hadiyth zenye amri na mafunzo muhimu ya maamkizi ya Kiislamu:
Tunapoingia majumbani mwa wenzetu:
((يَا
أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَدْخُلُوا بُيُوتًا غَيْرَ بُيُوتِكُمْ
حَتَّى تَسْتَأْنِسُوا وَتُسَلِّمُوا عَلَى أَهْلِهَا ذَلِكُمْ خَيْرٌ
لَّكُمْلَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ((
((Enyi
mlioamini! Msiingie nyumba zisio nyumba zenu mpaka muombe ruhusa, na
muwatolee salaam wenyewe. Hayo ni bora kwenu mpate kukumbuka)) [An-Nuur: 27]
Mifano kutoka kwa Malaika:
Kutoka kwa Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) alipoingia kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akiweko Mama wa Waumini:
عن
عائشة رضي الله عنه قالت: قال لي رسول الله صلى الله عليه وسلم:
((هذا جبريل يقرأ عليك السلام)) قالت: قلت: "وعليه السلام ورحمة
الله وبركاته" متفق عليه
Kutoka
kwa Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) kwamba Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliniambia: ((Huyu Jibriyl
anakutolea salaam)) Nikamjibu: "Wa ‘Alayhis-Salaam wa RahmatuLLaahi Wa Barakaatuh" [Al-Bukhaariy na Muslim]
Malaika walipopita nyumbani kwa Nabii Ibraahiym (‘Alayhis-Salaam) kuelekea mji wa Nabii Luutw (‘Alayhis-Salaam) kuuangamiza:
((هَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ ضَيْفِ إِبْرَاهِيمَ الْمُكْرَمِينَ))
((إِذْ دَخَلُوا عَلَيْهِ فَقَالُوا سَلَامًا قَالَ سَلَامٌ قَوْمٌ مُّنكَرُونَ))
((Je, Imekufikia hadiyth ya wageni wa Ibraahiym wanaoheshimiwa?
((Walipoingia kwake wakasema: Salaam! Na yeye akasema: Salaam! Nyinyi ni watu nisiokujueni)) [Adh-Dhaariyaat: 24-25]
0 comments:
Post a Comment