Feb 25, 2014

TUIKUMBUKE HISTORIA HII

 

Jumanne, Februari 25, 2014

Siku kama ya leo miaka 1067 iliyopita mwaka 368 Hijiria, alizaliwa mjini Cordoba, Uhispania, faqih, mtaalamu wa hadithi, fasihi na mwanahistoria Abu Omar Yusuf bin Abdullah, mashuhuri kwa jina la Ibn Abdul Barr. 

Alipata masomo ya msingi kutoka kwa baba yake na walimu wengine wakubwa wa kipindi hicho. Ibn Abdul Barr aliupa umuhimu mkubwa utafiti, ambapo kwa kipindi cha muda mfupi alikuwa miongoni mwa wasomi wakubwa mjini Andalusia. 

Kufuatia kukosekana amani na usalama katika mji wa Cordoba, Ibn Abdul Barr alilazimika kuhamia mji mwingine wa Daynah ambao kipindi hicho ulikuwa moja ya vituo muhimu vya elimu vya Andalusia, na huko alifanikiwa kuandika vitabu kadhaa. 

Miongoni mwa vitabu vya msomi huyu mashuhuri ni kile cha "Al Istiiab" ambacho kinahusu maisha ya masahaba wa Mtume Muhammad (saw).
 XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Na siku kama ya leo miaka 20 iliyopita Mzayuni mmoja aliyekuwa na misimamo ya kufurutu ada aliwashambulia na kuwamiminia risasi Waislamu waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala katika Msikiti wa Haram ya Nabii Ibrahim mjini al Khalil, Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kuua shahidi 29 miongoni mwao. 

Mauaji hayo yalitokea wakati Waislamu hao walipokuwa katika ibada ya funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. 

Waislamu wengine wengi walijeruhiwa katika shambulizi hilo la kikatili.

Mauaji hayo ambayo yalidhihirisha tena uhasama na chuki za Wazayuni wa Israel dhidi ya Waislamu, yalilaaniwa na Waislamu kote duniani. 

Ukatili huo ulizusha wimbi kubwa la machafuko katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina ambapo wananchi walizidisha mapambano dhidi ya maghasibu wa Tel Aviv. 

Israel ilimshika kwa muda na kumuachia huru mhalifu huyo katili kwa kisingizio kwamba alikuwa punguani!

0 comments:

Post a Comment