Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame amesema kuwa milipuko miwili imetokea Jumatatu mmoja katika eneo la mkahawa wa Mercury.
Kamishna huyo alifahamisha kuwa mlipuko mwingine ulitokea katika eneo la Mkunazini karibu na kanisa, ambapo mlipuko wa kwanza uliotokea jana Jumapili, eneo la Pangawe.
Mkuu huyo wa Polisi alisema hakuna maafa kama vifo wala majeruhi katika matukio yote matatu wala mali iliyoharibiwa:
“Isipokuwa watu walikumbwa na taharuki…walipigwa na butwaa na hofu kutokana na matukio hayo,” alisema Kamishna Hamdan.
Alisema upelelezi unaendelea ili kuwabaini wahusika wa miripuko hiyo. Hadi sasa hakuna watu waliyokamatwa, kutokana na matukio hayo.
Kuhusu hatua za tahadhari kufuatia miripuko hiyo, Kamishna Hamdan amesema Polisi imeimarisha ulinzi katika maeneo mengi ya Zanzibar.
Zanzibar kwa zaidi ya miaka miwili sasa, imekumbwa na matukio ya uhalifu wa kupindukia ikiwemo vifo, kujeruhi viongozi wa dini na wageni kwa kuwaunguza kwa tindi kali (acid) na kuharibu mali.
Hata hivyo, baadhi ya watu wanahoji kuhusu utendaji wa mamlaka za serikali zinazohusika na masuala ya sheria, kwa kushindwa kuwakamata wahusika wa kweli wa matukio ya uhalifu..
0 comments:
Post a Comment