Jan 10, 2014

Ndege za Kenya Zaua Wapiganaji wa Al Shabab

Shambulizi la anga lililofanywa jana na ndege za kijeshi za Kenya limeua wapiganaji kadhaa wa kundi la waasi la al Shabab huko kusini magharibi mwa nchi hiyo.

Habari hiyo imethibitishwa na Diyad Abdi Kalil ambaye ni miongoni mwa makamanda wa ngazi za juu katika jeshi la serikali ya Somalia. 

Amesema wapiganaji wasiopungua 11 wa kundi la al Shabab wameuawa katika shambulizi hilo la anga lililofanywa na ndege za Kenya dhidi ya kambi ya al Shabab katika mji wa Garbaharey ulioko kwenye eneo la Gedo.

Diyad Kalil amesema shambulizi hilo la jeshi la Kenya katika ardhi ya Somalia limefanyika kwa idhini na ushirikiano wa serikali ya Mogadishu.

Jeshi la Kenya liliingia Somalia mwaka 2011 kwa shabaha ya kupambana na wapiganaji wa kundi la al Shabab.

Shambulizi hili la anga la jeshi la Kenya limefanyika siku kadhaa baada ya serikali ya Somalia kutangaza kuwa inataka kukomboa baadhi ya maeneo yanayodhibitiwa na wapiganaji wa al Shabab.

0 comments:

Post a Comment