Jan 21, 2014

AULIWA KISHA AKATWA ZIWA

MWANAMKE mmoja aliyefahamika kwa jina la Agnes Peter amefariki dunia baada ya kukatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili na watu wasiojulikana na kisha kuondoka na titi lake la kushoto.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Leonard Paul, tukio hilo lilitokea Januari 18 mwaka huu saa 1:30 jioni katika Kitongoji cha Kilobe, Kkijiji cha Namsega, Kata ya Runzewe Magharibi, wilayani Bukombe.

Kamanda Paul alisema kuwa mwanamke huyo mkazi wa Namsega alifariki dunia papo hapo baada ya kukatwa mapanga  sehemu mbalimbali za mwili wake na wauaji hao kuondoka na titi lake la kushoto.

Alisema kuwa chanzo cha tukio hilo inasadikiwa kuwa ni mgogoro wa muda mrefu wa madai ya fedha uliokuwepo baina ya marehemu na mdai wa fedha hizo ambaye hajulikani alipo.

“Hadi sasa hakuna mtu anayeshikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kuwa mdai wa marehemu huyo alitoweka kusikojulikana na jeshi linaendelea na msako,” alisema.

Kamanda Paul aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano ili kufanikisha kukamatwa kwa wahusika wa tukio hilo.

0 comments:

Post a Comment