Nov 16, 2013

Tanzania Yadaiwa Kuwanyanyasa Wasichana-RIPOTI

Marekani imetoa ripoti inayozungumzia usafirishaji wa binadamu ya mwaka 2013, huku ikiitaja Tanzania kuwa kinara wa kunyanyasa wasichana, kuwatumikisha katika ngono na usafirishaji wa binadamu.
 

Ripoti hiyo iliyotolewa na idara ya nchi hiyo inayohusika na diplomasia (US Department of State, Diplomacy in Action), pia inaitaja Tanzania kuwa ni kitovu cha njia ya kusafirisha wanawake, watoto na wanaume ambao hutumikishwa kwenye kazi za mashambani na biashara ya ngono.

Ripoti hiyo iliyozinduliwa Julai  mwaka huu   na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Seneta John Kerry inaweka bayana kwamba biashara ya usafirishaji wa binadamu hufanywa na baadhi ya ndugu na marafiki ambao hutoa ahadi kwa wahusika kwamba wanakwenda kuwasomesha au kuwatafutia ajira nzuri mijini.

“Unyonyaji wa wasichana wadogo na utumikishaji majumbani ndilo tatizo linaloongoza, ingawa kesi za watoto kusafirishwa kwa ajili ya biashara ya ngono katika mpaka wa Tanzania na Kenya zinaongezeka. 

Pia, wasichana wananyonywa kwenye maeneo ya utalii,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watoto kutoka Burundi na Kenya, watu wazima kutoka Bangladesh, Nepal, Yemen na India wanatumikishwa kufanya kazi kwenye sekta za kilimo, madini na majumbani nchini Tanzania.

“Baadhi ya raia kutoka nchi  jirani huingia Tanzania kwa hiari yao, lakini hulazimishwa kufanya kazi majumbani kabla ya kupelekwa kutumikishwa kwenye biashara ya ngono Afrika Kusini, Ulaya na Mashariki ya Kati,” inaeleza.

0 comments:

Post a Comment