Oct 8, 2013

Wazee Wengi Wana Matatizo Ya Akili

SERIKALI imesema kuna wazee wengi wana tatizo la afya ya akili lakini hawajitambui kutokana na kutohudhuria vituo vya huduma za afya.

Kauli hiyo ya serikali ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, alipokuwa akitoa tamko kuhusu Siku ya Afya ya Akili Duniani, ambayo huadhimishwa Oktoba 7, kila mwaka. Kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Afya ya Akili kwa Wazee’.

Alisema wazee wengi wanakumbwa na hali hiyo kutokana na umaskini, kutengwa na jamii, kuwa tegemezi, upweke na upotevu wa vitu mbalimbali, mfano kufiwa na mtu wa karibu, kupoteza mali, kupoteza kazi au kuwa mlemavu.

“Sababu nyingine ni kukosa huduma muhimu, unyanyapaa na ubaguzi,” alisema.

Mbali na tatizo hilo, alisema magonjwa yanayoathiri wazee kwa wingi ni sonona, udhaifu wa fahamu, kisukari, saratani mbalimbali na shinikizo kubwa la damu na moyo.

Alisema magonjwa mengine ni ya kuchanganyikiwa, yanayohusiana na matumizi ya pombe, tumbaku na bidhaa zake, wasiwasi, matatizo ya kijamii ambayo nayo yanaonekana ni hali ya kawaida, hivyo huenda pasiwepo jitihada yoyote ya kupata msaada wa kitabibu.

Dk. Mwinyi alisema Tanzania ina wazee takriban 2,565,000 hivyo ifikapo mwaka 2050 tatizo hilo nalo litaongezeka.

“Taarifa ya afya na magonjwa ya akili ya 2012/13 inaonesha takriban wazee 13,789 wamehudhuria vituo vya huduma ya afya nchini. Idadi hii ndogo ya mahudhurio inachangiwa na uelewa mdogo wa jamii kuhusiana na matatizo mbalimbali ya afya ya akili kwa wazee,” alisema.

Kwa mujibu wa Dk. Mwinyi, ili kuboresha afya ya wazee, serikali kwa kushirikiana na wadau inapitia sera ya kuchangia gharama za afya kwa lengo la kufanya marekebisho ya vigezo vya utambuzi wa umri wa miaka 60.


0 comments:

Post a Comment