Takriban watu 18 wamefariki kwenye makabiliano makali kati ya
kundi la wapiganaji wa kiisilamu la Boko Haram na kundi la kijamii la kutoa
ulinzi kwa raia, katika jimbo la Borno Kaskazini Mashariki mwa Nigeria.
Wengi wa wale waliouawa waliaminika kuwa vijana wanaotoa ulinzi kwa
wanavijiji waliokuwa wanatoa ulinzi kwa mji wa Benisheik dhidi ya wapiganaji wa
kiisilamu.
Makabiliano hayo yametokea siku chache baada ya jeshi kufanya mashambulizi
dhidi kambi za Boko Haram na kuwaua wanamgambo 50.
Boko Haram linataka kuwepo kwa sheria za kiisilamu kote nchini Nigeria.
Kundi hilo limekuwa likifanya mashambulizi
makali sana
tangu mwaka 2009, ambayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu.
Lakini mashambulizi ya aina hiyo yameongezeka zaidi katika siku za hivi
karibuni licha ya jeshi kupeleka wanajeshi wake katika maeneo yaliyoathirika
zaidi.
Katika kujibu ongezeko la mashambulizi yanayofanywa na kundi hilo, Rais Goodluck
Jonathan alitangaza sheria ya hali ya hatari katika majimbo matatu Kaskazini
mwa nchi mnamo mwezi Mei likiwemo jimbo la Borno.
Aidha jeshi limeunga mkono ongezeko la makundi ya kutoa ulinzi
katika majimbo hayo ili kukabiliana na Boko Haram.