Umoja wa Mataifa umesema kuwa takriban wakimbizi elfu
25 kutoka Burundi wameondoshwa Tanzania kwa nguvu katika mwezi mmoja
uliopita.
Afisa wa shirika la Umoja wa Mataifa la
kuwahudumia wakimbizi UNHCR amesema malori yanayowasafirisha warundi
yamekuwa yakivuka mpaka kila siku , huku wahamiaji haramu wengi wakikosa
mahitaji muhimu kama vile maji na chakula
Katika wiki za hivi karibuni,
Tanzania imekuwa ikiwarejesha makwao kwa nguvu wale walioelezwa
wahamiaji haramu kutoka Burundi, Rwanda na Jamuhuri ya Kidemokrasi ya
Congo.
Kwa miaka mingi Tanzania iliwahifadhi mamilioni
ya wakimbizi waliokuwa wakiyakimbia mapigano katika nchi jirani .
Tanzania kwa upande wake inasema watu hao ni wahamiaji haramu wala sio
wakimbizi.
Takriban watu milioni moja walitoroka kutoka
Burundi na kuingia Tanzania wakati wa mgogoro wa wenyewe kwa wenyewe
wakati vita vilipozuka mwaka 1993. Wengi walirejea kwa hiari wakati
amani ilipopatikana mwaka 2006.
Nchi hiyo imekuwa makao kwa mamilioni ya
wakimbizi katika kipindi cha zaidi ya miaka kumi iliyopita kutokana na
migogoro katika eneo la maziwa makuu.
Maafisa wa Tanzania sasa wameanza kutekeleza
amri ya kuwaondoa kwa nguvu wale wanaodaiwa kuwa wahamiaji haramu kutoka
Burundi, Rwanda, na Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo.
Shughuli hii imetokea wakati mmoja na mgogoro wa
kidiplomasia kati ya Tanzania na Rwanda ambayo imekuwa ikikanusha madai
ya kuchochea vurugu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Mgogoro ndani ya Jamhuri ya kidemokrasia ya
Congo nao unaendelea kuchochea idadi ya wakimbizi wanaotoroka vita na
kuingia katika nchi jirani.
0 comments:
Post a Comment