Mar 19, 2016

Mshukiwa mkuu wa mashambulizi ya Paris akamatwa

Mshukiwa mkuu wa mashambulizi ya kigaidi ya Paris Salah Abdesalam amejeruhiwa na kukamatwa na maafisa wa usalama katika mji mkuu wa Ubelgiji, Brussels hapo jana Ijumaa katika msako mkubwa
Abdeslam mwenye umri wa miaka 26 na washukiwa wengine wanne walikamatwa katika mtaa wa Molenbeek mjini Brussels. 

Waendesha mashitaka wamesema mshukiwa huyo wa mashambulizi ya kigaidi yaliyofanyika mwezi Novemba mwaka jana katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris alijeruhiwa mguuni wakati wa operesheni hiyo ya polisi ya kumkamata.

Abdeslam anaaminika ndiye aliyapanga mashambulizi ya kujitoa muhanga katika maeneo mbali mbali mjini Paris ambayo yalisababisha vifo vya watu 130 na kusababisha watu wengine 350 kupata majeraha. Rais wa Ufaransa Francois Hollande amesema vita dhidi ya ugaidi havikomi baada ya operesheni hiyo ya jana jioni licha ya kuwa ni ushindi.

Hollande ambaye pamoja na Waziri mkuu wa Ubelgiji Charels Michel walifanya mkutano wa pamoja kwa wanahabari, amesema anawafikiria waathiriwa wa mashambulizi ya tarehe 13 Novemba kwasababu Salah Abdeslam alihusika moja kwa moja katika maandalizi, uratibu na kutekeleza mashambulizi hayo.
Salah Abdeslam Fahndungsfoto Salah Abdeslam amekuwa mafichoni kwa miezi minne
Rais huyo wa Ufaransa amesema ataomba Abdeslam kupelekwa Ufaransa kutoka Ubelgiji haraka iwezekanavyo ili kufunguliwa mashitaka. Hollande anatarajiwa kufanya mkutano wa baraza la ulinzi na usalama Jumamosi kufuatia kukamatwa kwa mshukiwa huyo ambaye alikuwa anasakwa kote barani Ulaya.

Michel ambaye alilazimika kuondoka ghafla kutoka mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya na Uturuki wa kujadili suala la wahamiaji, amesema kukamatwa kwa Abdeslam ni hatua muhimu sana kwa taifa lake katika vita dhidi ya kuenea kwa itikadi kali.

Mshukiwa mwinine aliyekamatwa katika operesheni hiyo ni mwanamume anayejulikana kwa jina bandia Amine Choukri ambaye pia anatumia jina jingine la kisyria la Monir Ahmed Alaaj.

Abdeslam na Choukri walichukuliwa alama za vidole na polisi wa Ujerumani mnamo tarehe 5 mwezi Oktoba, mwezi mmoja kabla ya mashambulizi ya Paris.Choukri pia anashukiwa kuwa Soufiane Kayal ambaye alisimamishwa na polisi katik mpaka kati ya Austria na Hungary mwezi Septemba wakiwa na Abdeslam.

Mshukiwa pekee wa mashambulizi hayo ya kigaidi ya Paris ambaye bado hajakamatwa ni Mohammed Abrini ambaye alinakiliwa katika kamera za uchunguzi katika kituo kimoja cha mafuta karibu na mji wa Paris siku mbili kabla ya kufanyika mashambulizi hayo.
Frankreich Paris Terroranschläge Trauer Watu 130 waliuawa katika mashambulizi ya kupangwa mjini Paris, Novemba 2015

Abdeslam ambaye ana rekodi ya uhalifu, anaaminika kuwa mshukiwa pekee aliye hai miongoni mwa timu ya majihadi 10 waliofanya mashambulizi ya kigaidi Paris wakiulenga ukumbi wa burudani wa Bataclan, mikahawa na uwanja wa michezo wa Stade de France.

Inasemekana mshukiwa huyo ambaye ni mzaliwa wa Ufaransa mwenye asili ya Kimorocco alitorokea Brussels siku moja baada ya mashambulizi hayo, baada ya kutojiripua na inaaminika tangu mashambulizi hayo, amekuwa katika mji huo wa Brussels.

Waendesha mashitika wamesema kikosi maalumu cha usalama kiliisaka nyumba moja katika mtaa wa Molenbeek kufuatia ushahidi uliopatikana katika operesheni nyingine iliyofanywa mjini Brussels siku ya Jumanne ambapo mshukiwa mwingine anayeshusishwa na mashambulizi ya Paris aliuawa na wengine wawili walitoroka.

Alama za vidole za Abdelslam ziligundulika katika nyumba hiyo na kupelekea msako mkubwa wa kumsaka. Vituo vya televisheni vya Ubelgiji vilimuonyesha Abdeslam aliyekuwa amefunikwa uso kwa kitambaa cheupe akiburutwa na maaskari kuelekea katika gari la polisi.

Rais wa Ufaransa amesema kufuatia kukamatwa kwa washukiwa kadhaa nchini Ubelgiji wanaohusishwa na mashambulizi ya Paris, kuna uwezekano mkubwa kuwa waliohusika walikuwa wengi kuliko ilivyokuwa inadhaniwa awali. Ubelgiji, hasa kitongoji cha Molenbeek kimetajwa kuwahifadhi wanajihadi wanaohusishwa na makundi ya wanamgambo wenye itikadi kali.

Abdeslam, Abdelhamis Abaaoud ambaye alikuwa mwanachama wa kundi la Dola la Kiislamu IS na mmoja wa washukiwa wakuu wa mashambulizi ya Paris na mshambulizi mwingine Bilal Hafdhi wote wanasemekana kuwahi kuishi katika mtaa huo.

0 comments:

Post a Comment